Katambi asema yuko tayari kuitwa msaliti

Muktasari:

Kiongozi huyo amesema kwamba kijana kwa upande wa upinzani ni kama karai kwenye ujenzi

Dar es salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi ambaye amehamia CCM amesema kama ataitwa msaliti basi atakuwa kundi la wasaliti wa nchi hii.

Akizungumza leo Jumanne mbele ya Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Katambi  amesema, “mambo mengi yalikuwa mrama  na watu tunapenda mabadiliko ila hatutaki kubadilika.”

"Kama nitaitwa msaliti basi nitakuwa msaliti kundi la wasaliti wa nchi hii, ukombozi ulishapatikana, siyo tunachokisema majukwaani ndiyo tunachokiishi,"

"Maisha tunayoyahubiri siyo tunayoishi, ukienda jimboni kwake, vijana kama nguvu kazi ya Taifa, tunajadili ‘personalities’ badala ya ‘issues’ mawazo mbadala," amesema.

"Niwaombe nijiunge na CCM siyo kwa sababu za madaraka ila tuijenge, CCM inatoa nafasi kwa vijana, vijana kwa upinzani ni sawa na karai katika ujenzi.”

Katika kikao hicho Rais Magufuli amesema karibu wanachama 200 wameomba kujiunga na chama hicho. Amesema kwa sasa hawatatambulishwa hadi mkutano mwingine.