CCM yajibu kauli za Lowassa, Zitto

Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka

Dar es Salaam. Siku chache baada ya aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa kuchambua matukio ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais John Magufuli, CCM imemjibu kuwa ni mpotoshaji na wala si tishio kwao.

Licha ya kumjibu Lowassa, CCM imesema Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amekuwa akiishambulia Serikali ya Awamu ya Tano kwa masilahi yake binafsi na imependekeza mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na wenyeviti wengine ambao chama hicho kinadai taasisi walizokuwa wanasimamia zimekumbwa na ufisadi mkubwa, wachunguzwe.

Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema jana kuwa Lowassa ni mpotoshaji na hoja alizotoa hivi karibuni kuhusu demokrasia na utumishi wa umma akifananisha hali ilivyo kuwa ni sawa na kaa la moto, zinamhukumu yeye mwenyewe.