Dk Bashiru Ally aeleza ukatibu mkuu utakavyomfunga

Muktasari:

  • Msimamo wake utategemea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM.

Dar es Salaam. Mwaka 2014 katibu mkuu mpya wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema Katiba ya sasa “haiwezi kuwa medani ya muafaka wa kitaifa kwa sababu ilisimamia msingi na muafaka wa kitaifa katika chama kimoja”, lakini usitegemee tena kumsikia akisimamia hilo.

Amebadili msimamo, sasa ‘anaganga yajayo’. Msimamo wake utategemea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM.

“Leo nazungumza kama katibu mkuu, yaani swali lako lina majibu humo humo,” alisema Dk Bashiru jana alipoongea na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam.

“Ukiwa mchambuzi, unachambua kweli kweli. Ukiwa msemaji wa chama, unawasilisha yaliyoamuliwa kwenye vikao.

“Halmashauri Kuu ndio chombo kikuu kilichoniteua na inaweza kunifukuza. Kwenye uchambuzi kule nisingeweza kufukuzwa.

“Hapa kama wewe unanitakia mema, siwezi kuchambua yale ambayo hayajaamuliwa na vikao. Lakini jambo kubwa nchi hii kama tutaheshimu katiba za vyama vyetu na Katiba za Serikali zetu mbili zilizopo, tunaweza kuanzia hapo kujadili namna ya kurekebisha Katiba hii.”

Dk Bashiru alionekana kuwa ni mpigania demokrasia na haki wakati akiwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akishiriki katika midahalo na mahojiano na vituo vya redio na televisheni kuhusu mijadala ya kitaifa.

Katika mitandao ya kijamii kumeenea kipande cha mahojiano aliyofanyiwa pamoja na Profesa Baregu katika kipindi cha Mizani ya Wiki cha televisheni ya Azam TV, wakati alipotoa msimamo unaoonekana kutofautiana na wa mwenyekiti wake, Rais John Magufuli. “Tangu mwaka 1992 wanasiasa wamekuwa wakidai Katiba mpya kwa hoja hiyo; kwamba tuko katika mazingira mapya ya kisiasa, mahitaji mpya ya kisiasa, tuna hatua mpya matarajio mapya, changamoto mpya, taratibu mpya za kuendesha nchi,” alisema katika mahojiano hayo.

“Lazima tuwe na medani mpya ya kujenga umoja wa kitaifa au mwafaka wa Kitaifa kwa hiyo Katiba ndiyo iwe medani ya mwafaka wa kitaifa siyo chama kimoja.

“Hiyo hoja haitakufa mpaka tumepata Katiba mpya.”

Kauli hiyo ni tofauti na msimamo wa Rais Magufuli, ambaye amesema kuandika Katiba mpya si kipaumbele chake.

Hata hivyo, Dk Bashiru alisema bado ni mtiifu wa katiba ya CCM na atakuwa mtiifu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na atatii historia ya mapambano ya ukombozi wa Tanzania.

Dk Bashiru alisema katika kipindi cha mwanzoni atatumia muda mwingi kujifunza hata jinsi ya kuzungumza na vyombo vya habari kupitia kwa katibu wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole tofauti na awali alipokuwa huru kujieleza kila alipoulizwa.

Kuhusu uanachama wake CCM, Dk Bashiru aliwataka waandishi kufuatilia siku aliyojiunga kwenye tawi ambalo hakulitaja.

“Ninachokuhakikishia kabisa ni kwamba nilipewa kazi hii nikiwa mwanachama wa CCM,” alisema.

Hataki siasa za majukwaani

Tofauti na mtangulizi wake , Abdulrahman Kinana aliyekuwa akizunguka mikoani kuongea na wafuasi wa chama hicho kwa kutumia mikutano ya hadhara, Dk Bashiru amesema kazi yake si siasa za majukwaani.

“Siasa za majukwaani ni mwenyekiti wa chama akisaidiwa na makamu wenyeviti wake wawili. Kule mikoani kuna wenyeviti wa vyama wa mikoa, wa wilaya, kuna wabunge na madiwani,” alisema Dk Bashiru.

“Ni marufuku kwa watendaji kufanya kazi ya siasa. Kazi ya siasa safi ni wale waliochaguliwa kwa miaka mitano. Sisi ni watendaji, naweza nikakaa nusu saa, naweza nikakaa saa moja, naweza nikakaa mwaka mmoja. Kwa hiyo kama mtendaji hamtaniona kwenye majukwaa kwa sababu wapo waliopewa dhamana ya kukaa kwenye majukwaa.”

Alisema kazi yake ni kubuni mikakati ya kutekeleza, kutoa taarifa kwenye vikao na kusimamia maelekezo ya chama.

Alisema mambo matatu atakayotekeleza katika sekretarieti ni bidii ya kazi, maarifa ya kutenda kazi na nidhamu.

Kinana

Akitoa maneno ya kumuaga, Kinana alimpongeza Dk Bashiru kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo. “Nimekuja hapa kumkabidhi ofisi na nimeshamkabidhi makabrasha yanayohusu ofisi. Nimepewa pia kazi ya kumtambulisha kwa watendaji, kazi zilivyokuwa zikifanyika. Nimewaomba watendaji wampe ushirikiano,” alisema Kinana.