Dk Bashiru asema ushindi wa CCM unazidi kushuka siku hadi siku

Muktasari:

Katibu huyo wa chama tawala amesema hivi sasa imekuwa vigumu kupata watu wa kupiga kura kwa sababu wananchi wanadharau uchaguzi na ushindi wao sasa hauzidi asilimia 40.

Morogoro. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema ushindi wa CCM unazidi kuporomoka siku hadi siku kutokana na wapigajikura kukosa imani na mifumo ya uchaguzi, ikiwa pamoja na vyama kutoa rushwa za mavazi na pesa.

Mbali na idadi ya wapigakura kupungua, Dk Bashiru amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ulizalisha Serikali isiyokuwa na uhalali wa kisiasa kwa kuwa watu wengi hawakujitokeza kupiga kura.

Dk Bashiru amesema hayo leo alipokuwa akitoa mada katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata) lililofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro mjini Morogoro, ambako alieleza kwa kina jinsi idadi ya wapigakura inavyozidi kupungua kutokana na tabia za vyama na wanasiasa.

 kuunda ushirika wa pamoja ili kuiwajibisha Serikali.

"Sasa wapigaji kura wajanja wa Tanzania wameanza tabia ya kudharau uchaguzi,” alisema Dk Bashiru mbele ya wakulima waliofurika kwenye ukumbi huo.

“(Wameanza tabia) Ya kukaa nyumbani kwa sababu wanaona ni kituko, ni mchezo wa kuigiza. Ndio maana leo kupata watu kwenda kupiga kura imekuwa shida. Note (angalia), tunakoshinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40. Hakuna mahali ambako wapigajikura wamejitokeza kwa asilimia 50," alisema Dk Bashiru.

"Na mwaka 2010 ulitia fora. Watu wengi walijiandikisha, kumbe walikuwa wanataka kile kiparata (kitambulisho cha mpigakura), kwa sababu kinatumika kwenda polisi kudhamini, kujitambulisha.

“Walipokipata wakaingia mitini. Kwa Mara ya kwanza katika historia ya nchi hii tulipata Serikali ambayo haina uhalali wa kisiasa kwa sababu wapigajikura wengi zaidi ya ailimia 50 walibaki nyumbani. Tatizo hili halijaisha, lakini wanasiasa wakishashinda, wanasema ameshinda hata kama ni kura moja. Hajali kwamba ushindi ule unatakiwa uwe na uhalali."

Alisema mfumo wa uchaguzi nchini umegubikwa na rushwa kiasi kwamba imefika mahali ambapo ukifika uchaguzi wagombea wanauza nyumba.

“Usipomchangia, anakuwa mkali utafikiri anakwenda kutibiwa,” alisema.

"Akishazikusanya fedha anakwenda kuwanunua wale mawakala na mawakala wanajua. Nao wanawanunua wapigaji kura. Msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi. Mnachotakiwa kufanya ni kubomoa na kuharibu soko la kura."

Alisema eneo jingine ambalo wanaweza kulitumia ni kuwawajibisha wote wenye vyeo kwa kuwa ni vya wananchi.

“Msichague kiongozi kwa T-shirt (fulana), kofia, kwa ubwabwa na kwa pesa. Kwa kufanya hivyo mnatengeneza watu wanaokuja kuwaonea,” alisema.

“Kwa sababu mamlaka ya Serikali yanatoka kwa wananchi. Vyeo vyote vilivyoko serikalini ni vyenu. Isipokuwa kuna mchakato wa kusimamia vyeo vyenu na moja ya michakato hiyo ni uchaguzi.

"Hebu tujiulize. Tabia na mwenendo wenu katika uchaguzi ukoje? Tuambizane ukweli, Mkishapewa kofia na T- shirt, halafu nyimbo zikaanza kupigwa za mbele kwa mbele, huwa mnahoji sifa ya mnayetaka kumchagua? Je, sifa ya chama kinachopiga mbele kwa mbele mnaijua?"

Kwa sababu dhuluma zote hazifanywi na wakoloni, bali wale mliowachagua.

Kuhusu masuala ya ushirika, Dk Bashiru alishauri wakulima kuunda ushirika wenye nguvu ili wawe na nguvu ya kuiwajibisha Serikali na kutetea masilahi yao.

Dk Bashiru alisema wakulima wanapaswa kuanzisha ushirika utakaowatetea katika masuala ya ardhi, mikopo na masoko.

 "Tuwe na Ushirika wa wananchi kudai haki za msingi kama ardhi. Kataeni kuuzwa kwa ardhi kama mnavyokataa kuuziwa damu. Tangu nimeingia ofisini, asilimia 99 ya malalamiko ni ya ardhi. Wengi ni masikini, matajiri wanakwenda wizarani. Mtafanywa watumwa kwenye ardhi yenu,” alisema.