Dk Bashiru awaonya wana CCM ‘wanaotema nyongo’ zao WhatsApp

Katibu Mkuu wa CCM,Dk Bashiru Ally (kulia) akisalimiana na Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani walipohudhuria kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 19 ya Mwalimu Julius Nyerere, lililofanyika Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere Kigamboni, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaonya makada wa CCM wanaopeleka malalamiko yao kwenye mtandao wa WhatsApp akisema watashughulikiwa kwa lengo la kukijenga chama.


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaonya wanachama wa chama hicho wanaohamishia mijadala ya chama kwenye mitandao ya jamii akisema watawajibishwa ili kukijenga chama hicho.

Ameyasema hayo leo Oktoba 10, 2018 wakati akichangia mjadala wa kumbukizi ya miaka 19 bila Hayati Mwalimu Julius Nyerere uliofanyika katika chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Huku akiutaja mtandao wa WhatsApp, Dk Bashiru amesema miongoni mwa mambo ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere ni dhana ya kujisahihisha huku akiwaonya wanachama wa CCM kupeleka malalamiko kwenye mitandao ya jamii.

“Sisi kama chama tumeruhusu mijadala kwenye vikao, badala ya kukaa kwenye mitandao ya WhatsApp. Atakayejadili masuala ya chama kwenye WhatsApp na akatapika nyongo na matusi, tutamshughulikia. Kwa sababu tunataka kujenga,” amesema Dk Bashiru.  

Amesema hakuna uhuru wa kudharauliana, kusema uongo, kuchocheana, kudhalilishana kwa kisingizio cha kujadiliana. “Hiyo haipo na mimi ndiyo msimamizi mkuu wa taratibu za chama, ujumbe umefika,” amesema.

Amesema, “lakini mijadala inayohusu kweli yenye dhamira njema watu wasiogope au kusingizia kwamba wanaogopa. Kwa nini ujifiche na jambo lako kama una nia njema. Kama umekosea utakosolewa kama mjadala,” amesisitiza.

“Lakini mijadala itatusahihisha, ndiyo maana Mwalimu aliweka dhana ya kujisahihisha. Katika nchi hii tumekosea mambo mengi. Tujadiliane tujisahihishe.”

Kuhusu uzalendo amesema uzalendo uliofundishwa na Mwalimu Nyerere ni wa kitaifa unaounganisha makabila, tamaduni na dini.

“Kwa hiyo tunapoanza kusifia uzalendo tuupe sifa. Uzalendo aliouhimiza Mwalimu ni wa kitaifa. Alitambua tunayo makabila mengi, tuna dini nyingi na tamaduni mbalimbali, lakini zote zikusanywe na utamaduni wa kitaifa, tujenge taifa,” amesema.

Amesema wananchi walipoacha kujadiliana masuala ukazuka uzalendo wa kibaguzi ukiwemo wa kikabila, kidini na wa kupenda vitu.

“Tuwe wakweli hii hali ipo na wakati mwingine imekuwa na wakati wa kutisha. Mtu anatafuta uongozi anaanza kuwasiliana na kabila lake. Au mtu anaangalia kabila lake limepunjwa au limezingatiwa,” alisema na kuongeza:

“Hivyo hivyo kwenye dini na siku hizi kuna ubaguzi hata wa kupenda vitu na anasa. Mtu anaiba lakini waliomchagua wanamwita jasiri, mjanja. Hiyo tukiizoea nayo inaweza ikawa uzalendo wa kusifu wezi.”