Jaji Mutungi, Profesa Lipumba washtakiwa rasmi mahakamani

File Photo

Muktasari:

Kesi hiyo namba 23 ya 2016 ilifunguliwa jana na Bodi ya Wadhamini wa CUF Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya Mahakama hiyo kuridhia maombi ya chama hicho ya kibali cha kumfungulia kesi msajili.

Dar es Salaam. Chama cha CUF kimefungua kesi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na msajili huyo, Profesa Ibrahim Lipumba.

Kesi hiyo namba 23 ya 2016 ilifunguliwa jana na Bodi ya Wadhamini wa CUF Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya Mahakama hiyo kuridhia maombi ya chama hicho ya kibali cha kumfungulia kesi msajili.

Wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wananchi 11 waliosimamishwa uanachama na CUF, akiwamo Naibu Katibu Mkuu (Bara) ambaye pia ni mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya.

Bodi hiyo inaiomba Mahakama itoe amri kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CUF.

Pia, wanaiomba Mahakama itoe amri kumzuia Msajili kufanya kazi nje ya mipaka ya kisheria wakati wa utekelezaji wa majukumu yake na kumzuia kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya chama hicho.

Wadhamini hao wa CUF wanawakilishwa na jopo la mawakili wanne, Twaha Taslima, Juma Nassoro, Halfani Daim na Hashim Mziray.

CUF imekuwa kwenye mgogoro wa uongozi baada ya Profesa Lipumba kuandika barua kutengua ya awali aliyoandika kujiuzulu uenyekiti Agosti 5, 2015. Uamuzi huo ulisababisha vikao vya juu vya chama hicho kumsimamisha pamoja na wenzake na baadaye kumvua uanachama.

Profesa Lipumba aliwasilisha malalamiko kwa Msajili ambaye aliiandikia barua CUF akieleza kumtambua kuwa ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho.

Maombi ya CUF yanaungwa mkono na hati ya kiapo ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif Hamad.