Uchunguzi walionaswa na nyara za Sh3.3 bil bado bado

Muktasari:

  • Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya kusafirisha meno ya tembo, kucha na mifupa ya Simba, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Januari 20119 na Mei 27, 2023 eneo la Msumbiji na Tanzania.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kusafirisha nyara za Serikali ikiwemo mifupa 1,107 ya Simba zenye jumla ya thamani ya Sh 3.3 bilioni, inayowakabili washtakiwa 12 wakiwemo waliokuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Washtakiwa hao ikiwemo kampuni ya usafirishaji ya AB Marine Products Ltd pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Airline Ltd, wanadaiwa kusafirisha nyara hizo kutoka Msumbiji na kwenda Tanzania, ambapo zilikuwa zinapelekwa Kuala Lumpur, Malaysia bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori wa nchini hizo mbili.

Wakili wa Serikali, Erick Kamala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Alhamisi Mei 2, 2024, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuangalia iwapo upelelezi wa shauri hilo umekamilika au laa.

Wakili Kamala amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, kuwa kutokana na upelelezi kutokukamilika, wanaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 28, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 28/2023 ni Abdulah Hamad (58) mfanyabiashara na mkazi wa Ubungo Maziwa. Wengine ni Meneja Mkazi wa Kampuni ya Airline Ltd, Roseline Achachi Wandera (43) mkazi wa Mikocheni, Kennedy Mwambeta na Noel Kasaro (41) Mratibu wa Mizigo na mkazi wa Tabata.

Pia wamo walinzi wawili wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Tito Mwabe (34) na Erasto Makinda (46), wakala wa mizigo Theresia Lukanga (40) na Abubakari Pazi (32) ambaye ni wakala wa mizigo kutoka kampuni ya Smart Ocean.

Pia yupo Haipeng Guo (34) mfanyabiasha na raia wa China, Yassir Husein (50) mfanyabiashara na mkazi wa Arusha pamoja na Peter Kikweka (50), ambaye ni mkazi wa Ukonga Mombasa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wakabiliwa na mashtaka 12. Kati ya mashtaka 12 yanayowakabili washtakiwa hao, mashtaka mawili ni ya kuongoza genge la uhalifu; mashtaka matatu ni ya kughushi; mashtaka manne ya kupatikana na nyara za Serikali, shtaka moja kujihusisha na nyara za Serikali na shtaka lingine ni kukutwa na mifupa ya simba kinyume cha sheria.

Miongoni mwa mashtaka hayo, ni shtaka la kwanza na la pili ambalo ni kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, ambapo inadaiwa kati ya Januari Mosi 2019 na Mei 27, 2023 katika uwanja wa Ndege wa Pemba uliopo mji wa Cabo Delgado Province nchini Msumbiji, washtakiwa walipanga genge la uhalifu kwa kupokea, kuuza na kusafirisha vipande 166 vyenye thamani ya dola za kimarekani 1,410,000 sawa na Sh3.2 bilioni mali ya Serikali, bila kuwa na kibali.

Washtakiwa pia, wanakabiliwa na shtaka la kukutwa na mifupa ya Simba, ambapo kati ya Januari Mosi 2019 na Mei 27, 2023 katika uwanja wa Ndege wa Pemba uliopo mji wa Cabo Delgado nchini Msumbiji, isivyo halali walikutwa na mifupa 1,107 ya Simba yenye thamani ya Sh61 milioni, kinyume cha sheria.

Pia wanadaiwa kujihusisha na kupatikana na nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo vipande  166 vyenye uzito wa kilo 236.82, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, tukio wanalodaiwa kulitenda Kati ya Januari Mosi, 2019 na Mei 27, 2023.

Vile vile, wanadaiwa kupatikana na meno 20 ya Simba na kucha 65 za Simba zikiwa na thamani ya Sh 57milioni, na kusafirisha samaki aina ya Kaa bila  bila kuwa na vibali.