Aliyefungwa miaka 22 kwa vipande 12 vya nyama ya swala aachiwa huru

Maria Ngoda baada ya kuachiwa huru leo Ijumaa, Februari 16, 2024
Muktasari:
- Maria alihukumiwa kifungo cha miaka 22, Novemba 3, 2023 na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Said Mkasiwa baada ya kumtia hatiani. Hukumu hiyo kuliibua mjadala kutokana na kithibiti kilichodaiwa kuwa alikutwa nacho na idadi ya miaka aliyohukumiwa.
Iringa. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa imemuachia huru, Maria Ngoda aliyehukumiwa kifungo cha miaka 22 jela kwa kukutwa na vipande 22 vya nyama ya swala.
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, Februari 16, 2024 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Elvin Mgeta aliyesema kutokana na hoja zilizowasilishwa na mkata rafani, Maria hana hatia na yupo huru.
Awali, Maria alihukumiwa kifungo cha miaka 22, Novemba 3, 2023 na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Said Mkasiwa baada ya kumtia hatiani. Kutolewa kwa hukumu hiyo kuliibua mjadala kutokana na kithibiti kilichodaiwa kuwa alikutwa nacho na idadi ya miaka aliyohukumiwa.
Makundi mbalimbali yalipaza sauti, huku baadhi wakitangaza kumpa msaada wa kisheria kukata rufani.
Baada ya uamuzi huo wa Jaji Mgeta uliomuweka huru, Maria amesema: "Asante Mungu, nawashukuru ndugu zangu kunipigania, mimi ni mama mjane na wanangu kwa kipindi hiki chote sijui walikuwa katika hali gani. Asante Mungu."
Awali, akisoma hukumu hiyo, Jaji Mgeta amesema hoja zilizo wasilishwa na upande wa warufani zina mashiko.
Miongoni mwa hoja hizo ni suala la Maria kukosa uwakilishi wa kisheria wakati kesi yake ya awali inaendeshwa, huku upande wa mashtaka ukiwa na mawakili sita.
Pia, Jaji Mgeta amesema hakukuwa na mnyororo mzuri wa utunzaji wa nyama ambayo inadaiwa kukutwa kwenye ndoo aliyokutwa nayo Maria.
Hoja nyingine ni suala la Maria kutosikilizwa ushahidi wake kwamba, nyama ile alikuwa amekabidhiwa na mtu aliyedai kwenda kufuata hela.
"Suala la Maria kukutwa kwenye eneo la tukio na kukutwa ndoo ambayo ilidaiwa kuwa na nyama ni vitu viwili tofauti. Maria alikataa ndoo sio yake na utetezi huo ulipuuzwa," amesema Jaji Mgeta.
Hivyo, hoja kwamba ushahidi wa mkata rufaa haukuzingatiwa, ilitiliwa maanani.
"Kwenye mashahidi mwingine, alisema ndoo ilikutwa mbele yake na mwingine, mrufani alikuwa amebeba ndoo," ameongeza.
Hoja nyingine iliyofanyiwa kazi mahakamani hapo ni kwamba haikuthibitika kuwa ni nyama ya swala na kuwa iliharibiwa bila utaratibu.

Mama mkwe wa Maria Ngoda, Elesia Nyigu akishukuru mwanae kuachiwa huru
Mama mkwe wa Maria, Elesia Chungu amesema katika kipindi chote cha mwanaye kuwa gerezani, hali ya watoto nyumbani kwake iliyumba kutokana na uchumi duni.
"Hali ya uchumi ilikuwa mbaya, mwanangu alikufa na mama yao ndio huyo alikuwa gerezani. Asante sana kwa msaada mpaka ametoka yuko huru," amesema Chungu.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Iringa, Zainab Mwamwindi amesema rufaa hiyo imemtendea haki Maria ambaye awali alihukumiwa kimakosa.
"Tangu mwanzo tunafuatilia kesi hii na jambo zuri ni kuwa ameshinda. Maria sasa yupo huru. Tutakwenda nyumbani kwake kuona anaanzaje maisha mapya baada ya kukaa gerezani," amesema Zainab.
Kiongozi wa Chama cha Mawakili Tanzania (TLS), Letisia Ntagazwa aliyekuwa miongoni mwa mawakili amesema hoja zao zilikuwa na mashiko na ndio maana Maria ameachiwa huru.
"Maria hakuwa na utetezi wowote na hatukuwa na taarifa kuhusu kesi yake, niwaombe wananachi wanaona kabisa wanakosa uwakilishi, wanakosa haki mahakamani waje," amesema Letisia.
Hatua kwa hatua kesi ya awali hadi hukumu
Shahidi wa kwanza, askari wa wanyamapori anayefanya kazi na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) alisema siku ya tukio alikwenda eneo hilo akiwa na watu wengine akiwemo askari mwenzake, Philomon Wambura.
Kabla ya kufika eneo hilo waliungana na askari polisi, John Shayo na mwenyekiti wa kijiji cha Isakalilo, Maisha Modest na walifika eneo hilo saa 8:15 mchana na kumkuta Ngoda akiwa na ndoo nyeupe na ilipofunguliwa ilikutwa na nyama hiyo.
Kwa upande wake, askari polisi mwenye namba G 4395, koplo Lubeya aliiambia mahakama kuwa yeye ndio alipewa jukumu la kumhoji na kuandika maelezo ya mwanamke huyo na baadae kielelezo kiliteketezwa kwa amri ya mahakama.
Shahidi wa tatu, Mkunde Maleko ambaye ni askari wanyamapori kutoka Tawa, alisema yeye ndio alipewa vipande 12 vya nyama hiyo ya swala na aliitambua kuwa ni ya swala na alifanyia tathmini ya thamani na kubaini ina thamani ya Sh904,757.1.
Kwa upande wake, shahidi wa upande wa mashitaka, Maisha Modest ambaye ni mwenyekiti wa kijiji alisema siku hiyo alipokea simu kutoka kwa polisi, John Shayi akimtaka wakutane na alipokwenda alimkuta na watu wengine watatu.
Baada ya kumtambulisha kwa watu hao, walikwenda katika nyumba ya mama Ziada Mpiluka na walikuta watu ambapo walijitambulisha na katikati ya watu hao ndipo walipokutana na Ngoda akiwa na ndoo nyeupe ikiwa mbele yake.
Alitakiwa kufungua ndoo hiyo na alipoifungua, yeye aliona vipande 12 vya nyama na alipoulizwa ni ya mnyama gani hakuwa anafahamu bali yeye alipewa tu na mwanamke mwingine aliyemtaja kwa jina la Kibuna Fute auze ili aiuze.
Yeye pamoja na timu hiyo ya maofisa wanyamapori ilikwenda hadi nyumbani kwa Kibuna, lakini hawakumpata na ndipo Ngoda alipokamatwa na maofisa hao na polisi waliokuwa wamefuatana na kujaza fomu ya kukamata nyama hiyo.
Shahidi wa tano, Koplo Owago wa Jeshi la Polisi mwenye namba F 8404 na ndiye alikuwa mtunza vielelezo ambapo alisema Novemba 20, 2022 alipokea kielelezo cha nyama ya Swala ambapo aliandaa nyaraka zilizowezesha kuteketezwa.
Kwa upande wake, shahidi wa sita, WP koplo Agnes, kwamba akiwa kituoni alimpokea afisa mmoja wa Tawa akiwa na Ngoda akiwa na kielelezo cha vipande 12 vya nyama ya swala ambayo Ngoda alielezwa kukamatwa nayo.
Utetezi wa Maria ulivyokuwa
Katika utetezi wake, mwanamke huyo alieleza ni kweli alikamatwa katika eneo hilo linalotajwa na upande wa mashtaka akiwa na ndoo ya plastiki na kwamba awali alimkuta nayo ndoo hiyo ikiwa na mwanamke mwingine.
Baadaye mwanamke huyo alimuaga anakwenda nyumbani kuchukua fedha, lakini baada ya dakika 15 tu kupita, aliona watu waliofutana na mwenyekiti wa kijiji wakija eneo lake na walimweleza wanatilia shaka kilichopo ndani ya ndoo.
Walimwambia aifungue ndoo hiyo, lakini akakanusha kuhusika nayo na kuwaambia kuwa ndoo hiyo ni mali ya Kibuna Fute na walimtaka awaonyeshe alipo, lakini akawaambia kuwa alikuwa amemwaga kuwa anakwenda nyumbani.
Aliwaambia maofisa hao kuwa mwenyekiti anamfahamu mwanamke huyo pamoja na nyumba anayoishi, aliambiwa afungue ndoo hiyo na baada ya kufunguliwa kwa ndoo hiyo, maofisa hao walimweleza kuwa yeye ndio mmiliki wa nyama hiyo.
Hukumu ya mahakama
Katika hukumu yake, pamoja na ushahidi mwingine, mahakama iliegemea maelezo ya ungamo yanayodaiwa yalitolewa na mshtakiwa mwenyewe kwa hiyari yake akikiri kukutwa na vipande hivyo 12 vya nyama ya swala.
“Nakumbuka tarehe 19.11.2022, saa 8:15 katika mtaa wa Isakalilo kata ya Isakalilo Manispaa na Mkoa wa Iringa wakati nipo kwa mama ziada nikiwa nauza nyamapori lakini hakunitajia ni nyama gani,”anaeleza.
“Vilikuwa ni vipande kumi na tatu na kimoja alichukua, lakini nilivyokamatwa navyo ni vipande 12 vya nyama pori ambavyo nilipewa na Kibuna Fute ili nimuuzie”, alinukuliwa Ngoda katika maelezo ya onyo aliyoandika polisi.
Hakimu Mkasiwa alisema katika maelezo yake hayo, mshtakiwa alikiri kukutwa na vipande hivyo 12 vya nyama ya swala na akashindwa kuonyesha mashaka yoyote kwa ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa mahakamani.
“Lakini pia mshtakiwa alishindwa kuwahoji kikamilifu mashahidi wa upande wa mashtaka kuhusiana na ushahidi wa kukutwa na vipande hivyo 12 vya nyama ya swala. Ni sheria kama shahidi hakuhojiwa ushahidi wake unapokelewa” alisema.
“Hivyo upande wa mashtaka umeweza kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuwa mshtakiwa alipatikana na vipande 12 vya nyama ya swala ambavyo ni nyara za Serikali kinyume cha sheria,” alieleza Hakimu Mkasiwa katika hukumu yake.
Kwanini miaka 22 sio faini
Kwa hiyo, mshtakiwa ametiwa hatiani kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali kama alivyoshtakiwa nalo kinyume cha kifungu 86(1)(2)(c) (ii) cha sheria ya uhifadhi wanyamapori ikisomwa pamoja na sheria ya uhujumu uchumi,”alisema.
“Adhabu kwa kosa la kupatikana na nyara ya Serikali imeelezwa kwenye hicho kifungu kuwa ni faini isiyopungua mara tatu ya thamani ya nyara au kifungo kisichopungua miaka 10 na kisichozidi miaka 20 au vyote pamoja,”alisema.
“Vinginevyo, katika mazingira husika kama ilivyoelezwa na sheria, adhabu kwa mtu anayepatikana na nyara za Serikali inaelezwa katika kifungu cha 60(2) cha sheria ya makosa ya kupangwa na uhujumu uchumi kama ilivyorejewa 2022”
Kifungu hicho kwa mujibu wa Hakimu, mtu akipatikana na hatia ya makosa ya uhujumu uchumi, kama lilivyo kosa la Ngoda, atatumikia kifungo kisichopungua miaka 20 jela na kisichozidi miaka 30 au vifungo vyote viwili.
“Sasa adhabu iliyotolewa na kifungu cha 60(2) cha sheria ya uhujumu uchumi ni kubwa kuliko inayotolewa na kifungu cha 86(1)(2)(c) (ii) cha sheria ya uhifadhi wanyamapori ya mwaka 2009 kama ilivyorekebishwa mwaka 2022”
“Kulingana na namna na mazingira ya kosa lilivyotendeka na kwa kuzingatia mwongozo wa utoaji adhabu Tanzania wa mwaka 2023, anayepatikana na hatia ya kupatikana na vipande 12 vya nyara ni kati ya miaka 20 na 24 jela”
Hakimu alisema kutokana na maombolezo ya mshtakiwa (mitigation) aliyotoa mahakamani kuwa ni mkosaji wa kwanza na ana wategemezi, hivyo anastahili kupunguziwa adhabu, mahakama imempunguzia hadi miaka 22 badala ya 24.