Rufaa ya mjane aliyefungwa kwa kukutwa na nyama ya swala yaanza kusikilizwa

Maria Ngoda akitoka mahakamani baada ya rufaa yake kuanza kusikilizwa
Muktasari:
- Jopo la mawakili wanane wamewasilisha hoja zilizowafanya wakate rufaa kupinga hukumu ya kifungo cha miaka 22 jela dhidi ya Maria Ngoda aliyekutwa na vipande 12 vya nyama ya swala.
Iringa. Rufaa ya Maria Ngoda aliyehukumiwa kifungo cha miaka 22 jela kwa kosa la kukutwa na vipande 12 vya nyama ya swala imeanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu, mkoani Iringa.
Katika rufaa hiyo inayosimamiwa na Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), mawakili wanane wa mkata rufaa wamewasilisha hoja zilizowasukuma kufanya hivyo wakipinga hukumu hiyo iliyotolewa Novemba 3, 2023.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Said Mkasiwe alimhukumu Maria ambaye ni mjane na mkazi wa Isakalilo, manispaa ya Iringa kifungo cha miaka 22 jela baada ya kumtia hatiani.
Rufaa hiyo imegusa nyoyo za wakazi wengi wa Iringa ambao wamemiminika mahakamani ilifunguliwa baada ya hukumu ya Maria kuwa gumzo mitandaoni kama adhabu aliyopewa ilikuwa sahihi au la.
Akizungumza nje ya Mahakama leo Februari mosi, 2024, Wakili Moses Ambindwile amesema kilichofanyika mahakamani hapo ni upande wa mkata rufaa kuelezea hoja zilizowafanya wafikie hatua hiyo.
Miongoni mwa hoja zilizowasilishwa ni kwamba mkata rufaa hakutendewa haki ya kupewa msaada wa kisheria hasa kutokana na hali yake kiuchumi.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kusikiliza rufaa ya kesi ya Maria Ngoda aliyehukumiwa miaka 22 jela baada ya kukutwa na vipande 12 vya nyama ya swala
Imedaiwa Mahakama ilipaswa kuwasiliana na taasisi zinazotoa msaada wa kisheria, ili mkata rufaa atetewa wakati wa kesi yake.
Hoja nyingine iliyotolewa ni kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa vile vilikuwa vipande vya nyama ya swala.
Wakili Moses amesema vipo vigezo vinavyotumiwa na wataalamu wa kutofautisha nyama ambavyo katika kesi hiyo, havikutumika.
Mbali na hilo, mawakili hao wamedai hakukuwa na maelezo yaliyoonyesha kwamba baada ya ndoo ya mama huyo kukamatwa na nyama ya swala ni wapi ilihifadhiwa mpaka siku ya pili ilipowasilishwa.
Pia, wamedai kuwa ni haki ya mtuhumiwa kuulizwa ikiwa anajua kusoma au kuandika, ili maelezo yake aandike mwenyewe au kuandikiwa jambo ambalo halikufanyiwa kazi.
Hoja nyingine iliyo wasilishwa mahakamani hapo ni kwamba, maelezo ya mtuhumiwa yanatakiwa yachukuliwe ndani ya saa nne baada ya kukamatwa.
Lakini katika kesi hiyo mtuhumiwa alikamatwa saa 8.15 mchana akiwa Isakalilo, alifikishwa mahabusu saa 10.00 jioni ya Novemba 19, 2023, lakini maelezo alichukuliwa kati ya saa 2.00 hadi saa 3.00 asubuhi Novemba 20, 2023.
Hata hivyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Elvin Mgeta ameahirisha kesi hiyo mpaka kesho Ijumaa Februari 2, saa tatu asubuhi ambapo upande wa mawakili wa Serikali watawasilisha hoja zao.
Amedaiwa kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa waliomba kuongezewa muda wa kuandika maelezo hayo.
Mawakili hao waliiomba Mahakama hiyo iruhusu rufaa dhidi ya Maria na kumwachilia huru.
Kesi hiyo iliyo chini ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Elvin Mgeta itaendelea kusikilizwa kesho Februari 2 kwa mawakili upande wa Serikali kutoa maelezo yao.
Jopo la mawakili wanaomtetea Maria ni Jane Massey, Cosmass Kishamawe, Innocent Kibadu, Barnabas Nyalusi, Leticia Ntagazwa, Joshua Chusi na Mwanasheria wa UWT, Marijan Salehe.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Iringa, Zainab Mwamwindi amesema wakati huu ambao kesi inaendelea wamekuwa wakitoa huduma kwa watoto Maria na ni maombi yao aachiwe huru.