Kamati ya Bunge yaona madudu mradi wa NSSF

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeeleza kuthibitisha madudu katika utekelezaji wa mradi wa nyumba za kisasa wa Dege Eco Village Kigamboni ambao  ujenzi wake umesimama.

Mradi huo  ulikuwa unaendeshwa kwa pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambayo inamiliki asilimia 45 za hisa na kampuni ya Azimio Housing Estates (AHEL) inayomiliki asilimia 55.

Jana, mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka amesema kamati hiyo imeikabidhi Ofisi ya Bunge ripoti ambayo pia ina mapendekezo kwa ajili ya hatua zaidi.

Kaboyoka amesema ripoti hiyo imesheheni mambo mengi ambayo alikataa kuyataja akisema wakati ukifika yatatajwa.  “Ifahamike ni madudu sana ambayo yanakera.”

Mradi wa Kigamboni una thamani ya Dola 653,436,675  za Marekani (Sh1.3 trilioni).

Awali, kashfa hiyo iliibuliwa katika ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 na gazeti hili kuianika katika habari mfululizo.