Maporomoko ya tope yafunika nyumba 13 Muleba

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Maporomoko ya matope kutoka Mlima Kabumbilo hadi mwalo wa Kabumbilo yalianza kujitokeza Aprili 17, 2024 na awali iliripotiwa kwamba nyumba moja na ekari 10 za mashamba viliathiriwa.

Muleba. Maporomoko ya matope katika Mlima Kabumbilo Kijiji cha Ilemela wilayani Muleba yamefunika nyumba 13 wananchi wakizuiliwa kufika eneo hilo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Aprili 29, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga amesema nyumba 13 zifunikwa na matope yaliyoporomoka kutoka Mlima Kabumbilo

Mlima huo upo kwenye vitongoji vya Bushabo na Kabumbilo katika Kijiji cha Ilemela, Kata Gwanseli wilayani Muleba Mkoa Kagera.

Dk Nyamahanga amesema mpaka mchana wa leo hakuna majeruhi wala vifo vitokanavyo na maporomoko hayo.

Amesema wananchi wote walishapewa taarifa za kuhama katika eneo hilo na kwa sasa hakuna mtu anayetakiwa kuendelea kuishi au kwenda eneo hilo, maana ni eneo hatarishi.


New Content Item (1)
New Content Item (1)


Mkuu wa wilaya amesema wataalamu wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha madhila hayo.

“Nyumba 13 zimefunikwa na matope, mashamba ya watu yamefunikwa tumetuma Jeshi la Polisi kuzuia eneo hilo, ni marufuku wananchi kwenda huko, wakae mbali na eneo hilo ni hatari. Kuna mambo unaweza kukimbia kuangalia ila huko wasiende,” amesema Dk Nyamahanga

Zainabu Hamza, mkazi wa Bushabo amesema nyumba yake imefunikwa na matope, migomba na mazao mengine pia vimefunikwa na tayari familia yake ameihamisha kutoka eneo hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji Cha Ilemela, Chirisant Marchades amesema kila wakati kasi ya kasi inaongezeka, yanazidi kufunika makazi na mazao na kwamba kuna hatari ya uharibifu zaidi wa nyumba nyingine kufunikwa.

Amesema Kitongoji cha Kabumbilo kina nyumba 275 na watu 1,225 wanaishi humo na eneo lililoathiriwa lina nyumba 45, kati ya hizo nyumba 13 zimefunikiwa na matope.

Marchades amesema katika kuhakikisha familia zinapata sehemu ya kujihifadhi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muleba imewapatia mabati 90 ili kuwasaidia waliokumbwa na madhila hayo.

Ameiomba Serikali iendelee kuongeza ulinzi maana watu wanazidi kuwa wengi wanaokwenda kwenye eneo hilo ambalo lina hatari kubwa.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kagera, Zabron Muhumha amesema watu wote wanatakiwa kuhama kwenye  mazingira hayo, maana udogo na matope vinazidi kuporomoka.

“Kwa sasa hatakiwi mtu yeyote kuwepo, wasubiri tamko la Serikali,” amesema.

Maporomoko ya tope kutoka Mlima Kabumbilo hadi mwalo wa Kabumbilo yalianza Aprili 17, 2024 ndipo mkuu wa wilaya aliwataka wananchi kuhama eneo hilo, baada kuliripotiwa kwamba nyumba moja na eka 10 za mashamba kuathiriwa.