Kesi ya Lema yawa kaa la moto kwa wanasheria

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Muktasari:

  • Wakili Mfinanga alijitoa ghafla jana kuendelea na kesi hiyo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa shauri hilo.
  • Hatua ya kujitoa kwa wakili huyo inakuja ikiwa ni miezi mitatu baada ya Hakimu Kisinda aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, kujitoa kutokana na kuwekewa pingamizi na Jamhuri kuwa ana urafiki na mke wa Lema, Neema Lema.

Arusha. Ikiwa ni miezi mitatu tangu Hakimu Patricia Kidinda ajitoe kusikiliza kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ya kumkashifu Rais John Magufuli, Wakili wake, Sheck Mfinanga naye amejitoa.

Wakili Mfinanga alijitoa ghafla jana kuendelea na kesi hiyo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa shauri hilo.

Hatua ya kujitoa kwa wakili huyo inakuja ikiwa ni miezi mitatu baada ya Hakimu Kisinda aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, kujitoa kutokana na kuwekewa pingamizi na Jamhuri kuwa ana urafiki na mke wa Lema, Neema Lema.

Wakili Mfinanga alijitoa jana mbele ya Hakimu Desdery Kamugisha huku akitaja moja ya sababu kuwa ni kutokana na upande wa utetezi kutopewa jalada la mwenendo wa kesi licha ya kuliomba mara tatu mahakamani hapo.

“Kwa sababu nimeshaleta notisi ya kukata rufaa naomba kuingia kwenye rekodi najitoa kuendelea kumwakilisha mteja wangu kutokana na ninachokiona kisheria kwamba tumeomba proceedings (mwenendo) na imeshindikana, mimi siyo wakili wake tena nimejitoa,” aliiambia mahakama

Baada ya ombi hilo, Wakili Mfinanga alionekana akikusanya nyaraka zake na kuagana na mteja wake kisha kunyanyuka kwenye kiti alichokuwa ameketi na kutoka nje ya mahakama.

Lema atema nyongo

Kutokana hatua hiyo, Hakimu Kamugisha alimpatia nafasi Lema kuongea, alisimama na kutamka kuwa amemsikiliza wakili wake na hana pingamizi juu ya uamuzi wake.

Hata hivyo, Lema aliiambia mahakama hiyo kuwa kwa ufahamu wake hiyo ni mara ya tatu upande wa utetezi umeomba jalada la mwenendo wa kesi hiyo lakini hawajapewa, kwa sababu hiyo hana imani na hakimu.

Lema aliomba kupatiwa nyaraka zote katika kesi hiyo sanjari na muda wa kumtafuta wakili mwingine.

Naye Wakili wa Serikali, Khalili Nuda alisema ni haki ya kikatiba ya mshtakiwa kuwakilishwa mahakamani, hivyo ampatiwe muda wa kutafuta wakili mwingine.

Wakili Nuda aliimbia mahakama kuwa alikuwa umemleta shahidi wa kwanza Inspekta wa Polisi, Aristides kuanza kutoa ushahidi

Hakimu Kamugisha alisema mshtakiwa ana haki ya kupata mwakilishi wa kisheria.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14 itakapoanza kusikilizwa.