Kesi ya kupinga ving’amuzi kufungwa yaanza Iringa

Muktasari:
- Mara baada ya kuanza, mwanasheria wa Serikali, Mwinyiheri Aristaric aliiomba Mahakama hiyo, kutupilia mbali maombi hayo.
Iringa. Kesi ya kupinga kuondolewa kwa chaneli za ndani kwenye ving’amuzi vya Azam, Dstv, Zuku na Star times iliyofunguliwa na watu watano imeanza kusikilizwa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.
Mara baada ya kuanza, mwanasheria wa Serikali, Mwinyiheri Aristaric aliiomba Mahakama hiyo, kutupilia mbali maombi hayo.
Mwanasheria huyo alidai mbele ya Jaji Penterine Kente anayesikiliza kesi hiyo kwamba waleta maombi hao wameshindwa kuainisha ni kipengele gani cha sheria kilichowaongoza kupeleka maombi hayo.
Alidai kuwa maombi hayo yalipaswa kuwasilishwa kwa kutumia kifungu cha 19(2) (3) cha sheria inayopatikana katika sura ya 310 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho.
Alisema sheria hiyo inaitaka Mahakama kusikiliza maombi hayo ndani ya siku 14, lakini imeshindwa kufanya hivyo kutokana na baadhi ya wajibu maombi kutokuwapo mahakamani baada ya waleta maombi kushindwa kuwafikishia samansi kwa wakati.
Akijibu hoja hizo, wakili wa upande wa waleta maombi, Edmund Mkwata alisema Mahakama haifungwi na sheria kutosikiliza maombi hayo katika hatua za awali kwa sababu ya baadhi ya wajibu maombi kutokuwapo mahakamani, badala yake alidai kuwa sheria inahitaji wajibu maombi wawepo kama Mahakama itaona kuna ulazima wa kuwapo.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Multichoice (T) Ltd kupitia king’amuzi cha Dstv; Simba Net (T) Ltd ambao ni wamiliki wa Zuku; Azam TV; Starmedia (T) Ltd, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA); Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baada ya kusikiliza uwasilishaji wa pande zote mbili, Jaji Kente aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 10 atakapotoa uamuzi wa kama Mahakama itasikiliza maombi hayo au itayatupilia mbali.
Katika kesi hiyo namba moja ya mwaka 2018, waleta maombi Silvanus Kigomba, Jesca Msambatavangu, Oliver Motto, Sebastian Atilio na Hamdun Abdallah, wameiomba Mahakama Kuu kubatilisha amri ya kuondolewa chaneli za ndani kwenye ving’amuzi vya Azam, DSTV, Zuku na Startimes ili kutoa nafuu kwa watumiaji wa ving’amuzi hivyo kuendelea kupata matangazo ya chaneli za ndani.
Akizungumza nje ya Mahakama, Msambatavangu aliishukuru mahakama kwa kupokea na kuanza kuisikiliza kesi hiyo akisema anaimani kwamba haki itatendeka.