Kilango akutana na hasira za JPM siku 30

Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela.

Muktasari:

Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu kuteuliwa kwake.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu kuteuliwa kwake.

Aliteuliwa Jumapili ya Machi 13 na jana Jumatatu alikuwa anatimiza siku ya 30 hivyo kama ni mshahara, atakuwa amepata wa mwezi mmoja tu.

Kilango ambaye alikuwa mtu wa 19 kushika wadhifa wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga tangu uhuru, uteuzi wake umetenguliwa kutokana na kushindwa kusimamia vyema upatikanaji wa watumishi hewa kwenye mkoa wake.

Sambamba na Kilango, Rais pia ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul Dachi kwa kushindwa kumsaidia mkuu wa mkoa kutafuta taarifa za kutosha juu ya uwepo wa watumishi hewa.

Akizungumzia uamuzi huo, Dachi alisema ameupokea kwa sababu Rais ndiye mteule wake huku akisema taarifa ya watumishi hewa waliyoipeleka Ikulu ina mambo yote.

Rais amechukua uamuzi huo baada ya kutuma timu Shinyanga kuhakiki watumishi na kubaini kuwa 45 ni hewa huku zikiwa zimebaki wilaya mbili; Shinyanga Vijijini na Kishapu kuhakikiwa.

Akizungumza Ikulu, jana wakati akipokea taarifa ya mwaka ya Takukuru, Rais Magufuli alisema wafanyakazi hao tayari walikuwa wamelipwa mshahara jumla ya Sh339.9 milioni kwa mwezi uliopita.

“Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni ziro, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini mkuu wa mkoa alisema hakuna mtumishi hewa? Alisema.

Rais Magufuli alisema baada ya kutengua uteuzi wake, Kilango atapangiwa kazi nyingine huku akiwataka wakuu wa mikoa yote kuwafichua watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja. Pia, ameagiza timu iliyofanya uchunguzi Shinyanga ifanye hivyo katika mikoa mingine, wizara na taasisi yoyote.

“Nilijiuliza sana kwa nini mkuu wa mkoa alisema katika mkoa wake hakuna watumishi hewa wakati nilisema hakuna adhabu? Huenda Ras (katibu tawala wa mkoa) alimdanganya lakini alishindwa kuchukua hatua zaidi kuona anachoambiwa ni kweli au la?,” alihoji Dk Magufuli.

Alisema mpaka sasa kuna wafanyakazi 5,507 nchi nzima ambao wamelisababishia Taifa hasara ya zaidi ya Sh53 bilioni na kufafanua kwamba kwenye Serikali za Mitaa wapo zaidi ya 4,200 na Serikali Kuu 1,300.

Hata hivyo, hivi karibuni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Angela Kairuki alikaririwa akisema kwamba watumishi hewa waliobainika nchi nzima ni 7,795 ambao wameisababishia Serikali hasara ya Sh7.5 bilioni.

“Ninaomba Chief Secretary (Katibu Mkuu Kiongozi), timu yangu hii itafutiwe ulinzi mzuri ili kila nitakapowatuma wafanye kazi yao vizuri,” alisema.

Alisema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha, Serikali imeongeza fedha za maendeleo kutoka asilimia 26 mpaka 46 ili kuwaletea maendeleo wananchi.

“Nimesikia kuna makatibu wakuu wanalalamika kwamba tumepunguza OC (matumizi mengine) kwenye bajeti ijayo, kama hawataki waache kazi. Wapo pia na mawaziri wanalalamikia OC nao nawatafuta niwajue ni akina nani, naona mindset (dhana) bado haijabadilika,” alisema na kusisitiza kwamba Serikali yake imejipanga kufanya mambo ya maendeleo kwa kupunguza matumizi yasiyo ya msingi.

Alisema katika bajeti ijayo Serikali imepanga kununua ndege tatu, meli mpya na vifaatiba ili wagonjwa watibiwe hapahapa nchini.

 

Alichosema Kilango

Alipoulizwa taarifa za kushindwa kwake kubaini watumishi hewa hadi kutenguliwa uteuzi wake, Kilango alikataa kuzungumzia suala hilo:

Mwananchi: Mheshimiwa, leo Rais ametengua uteuzi wako kwa sababu ulishindwa kuwapata watumishi hewa katika mkoa wako. Tatizo lilikuwa wapi?

Kilango: Nani amekupa taarifa hizo?

Mwananchi: Rais mwenyewe amesema.

Kilango: Aliitisha Press Conference?

Mwananchi: Alikuwa anachomekea tu wakati anapokea ripoti ya Takukuru

Kilango: Basi, siwezi kuzungumza. Wewe ndiyo mtu wa kwanza kunipa taarifa. Asante.

Hata hivyo baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga walisema baada ya kusikia taarifa hizo, Kilango alishtuka na kudai kuwa watumishi waliompa taarifa ya kuwa hakuna watumishi hewa wamemponza.

Watumishi hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe walisema, Kilango alikuwa ofisini kwake akiangalia televisheni lakini baada ya muda alimuagiza mtumishi mmoja amwite katibu tawala lakini hawakujua walichozungumza.

 

Alivyoingia Shinyanga

Aprili 5, Kilango alikaribishwa rasmi katika Mkoa wa Shinyanga kwa sherehe iliyofanyika katika Uwanja wa Shycom ambako alieleza vipaumbele vyake.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa, dini na kimila, Kilango aliwaambia wananchi hao kuwa yupo Shinyanga kwa ajili ya kumsaidia Rais Magufuli kuwaletea maendeleo wananchi kwa kutekeleza kaulimbiu ya ‘Hapa kazi tu’.

Kilango alipewa jina la Mbula ambalo ni la kiongozi mkubwa wa kimila. Mbula anadaiwa kwamba alikuwa mganga wa 33 kati ya 54 maarufu nchini.

Katika sherehe hizo pamoja na mambo mengine wazee wa kimila (machifu) wa Kabila la Kisukuma walimsimika Kilango kuwa chifu wa Kisukuma na walimkabidhi zana mbalimbali za kimila ili azitumie katika uongozi wake.

 

Kabla ya uteuzi

Kilango aliwahi kuwa Mbunge wa Same Mashariki lakini alishindwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.

Pia, amewahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika Serikali ya Awamu ya Nne.

 

Wasomi waunga mkono

Wakizungumzia hatua hiyo, wasomi na wanazuoni nchini wamepongeza uamuzi wa Dk Magufuli wa kutengua uteuzi wa Kilango wakisema kada huyo amefeli mtihani wa kwanza aliopewa na Rais siku aliyoapishwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk Benson Bana alisema wazo la kwanza alilolipata baada ya kupata taarifa hizo ni dalili nzuri ya uwajibikaji kwa upande wa Rais.

Alisema Dk Magufuli hataki mambo ya danganya toto kwenye masuala ambayo ni magumu na nyeti kwa Taifa, hataki majibu mepesi mepesi hivyo lazima wakuu wa mikoa watume taarifa sahihi wafanye kazi ya kutosha wajiridhishe katika kutoa majibu yao.

“Wanasiasa wetu walijue hili... inabidi viongozi wetu wanapoamua kufanya mawasiliano wajiridhishe kwanza, kwa taarifa ambazo zina upembuzi yakinifu wapate ukweli wazungumze ukweli Watanzania wanataka kuambiwa ukweli na si blabla,” alisema Dk Bana.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa UDSM, Elijah Kondi alisema Kilango amejifukuzisha mwenyewe kwa kushindwa kutimiza jukumu alilopewa.

“Tukumbuke kwamba wakati Rais alipowateua alitoa pia ahadi kwamba kwa wale ambao hawatatekeleza majukumu yao atashughulika nao kwa hiyo mimi nachukulia uhalisia wa namna Rais anavyolishughulikia suala la uwajibikaji,” alisema Kondi.

Alisema labda kama kuna jingine ambalo wengi hawalijui, lakini kitu ambacho kila Mtanzania anakijua ni kwamba Rais alitoa majukumu kwa kila mkuu wa mkoa, alisisitiza kuwajibika katika mapana yake.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Richard Mbunda alisema ni wazi kwamba Rais hataki viongozi anaowateua katika hizo nafasi wafanye kazi kwa mazoea, maana wengi walishazoea kwamba wakishateuliwa wanastarehe.

Alisema huo ni ujumbe tosha, kwani alitoa agizo wakati anawaapisha kwamba waende wakaanze na watumishi hewa. Aliwataka viongozi wengine wajiandae na kwamba wakifanya makosa rungu litawashukia

“Hili ni onyo kisiasa, walioteuliwa wanapaswa kuanza kujiona kwamba ukishapewa uteuzi si kwamba umeula, ila kubaki kwako madarakani kutategemea utendaji kazi ambao utawafurahisha siyo tu wananchi, bali hata waliokuteua akiwamo Rais mwenyewe,” alisema Mbunda: “Pili inaonyesha kabisa kwamba kuna wale viongozi au kada ya zamani ndiyo naiona kama inaanza kuondoka, wale ambao walizoea kufanya kazi kwa mazoea tunaona kwamba wanaanza kuondoka kwa sababu hawawezi kwenda na kasi ya Rais.”

Mkazi wa Shinyanga, Athanas Emmanuel alipongeza uamuzi wa Rais akisema ni sahihi kwani Kilango alitakiwa atoe taarifa sahihi.

Lakini Joseph Richard pia wa Shinyanga alisema Rais angewaonya kwanza na kuwataka wafanye uchunguzi kwa makini badala ya kutengua uteuzi.

 

Nyongeza na Harieth Makwetta na Suzy Butondo