Mbowe asisitiza muungano wa Serikali tatu

Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe akiongoza maandamano ya amani. 

Muktasari:

  •  Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesisitiza msimamo wa chama hicho ni kuwa na muungano wa Serikali tatu,  ikiwamo Serikali ya Tanganyika.

Musoma/Dar. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema licha ya muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kutimiza miaka 60, bado unahitaji maboresho, akipendekeza muundo wa Serikali tatu ikiwamo ya Tanganyika.

Mbowe ameyasema hayo jana Aprili 26, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Musoma mkoani Mara, akisisitiza msimamo wa chama chake wa kuunga mkono uwepo wa serikali tatu kama ambavyo ilipendekezwa na tume ya Jaji Joseph Warioba.  

"Naomba mtuelewe vizuri sisi sio kwamba hatuutaki Muungano, tunautaka na tunaupenda ila tunachotaka ni utaifa wetu utambulike kama ilivyo kwa wenzetu kwa sababu wao licha ya kuwa ni wachache, lakini wana serikali yao, wana bunge lao na wana rais wao sisi vya kwetu viko wapi?

"Tunataka Tanganyika tubaki na Tanganyika yetu na serikali yetu kama ilivyo kwa Wazanzibari, kisha tunaunda Serikali ya Muungano, pia naomba mjue kuwa sisi Chadema hatutaki siasa za kibaguzi ila tunataka muungano unaotambua haki za pande zote mbili,” amesema.

Amesema Watanzania lazima wasimame wadai mabadiliko ili kuondokana na changamoto za maisha, huku akidai kilio cha maisha magumu hivi sasa kiko kila sehemu nchini.

"Unafikiri rais au waziri mkuu anajua kama maisha ni magumu? Wao wataelewaje wakati wanalipiwa kila kitu na mishahara minono juu, kwa hiyo ndugu zangu tunachokitaka sisi Chadema ni kuondokana na hizi shida naamini hata wana CCM wenye akili timamu watatuunga mkono kwenye hili," amesema.

Awali akizungumza kwenye  mkutano huo, kada wa Chadema, Mdude Nyangali amesema maandamano ya chama hicho yanalenga kumkomboa Mtanzania ambaye amekuwa katika hali ngumu kimaisha licha ya Tanzania kubarikiwa rasilimali nyingi.

"Tunaandamana tukitaka Serikali ishushe gharama za maisha kwani vitu vimepanda bei sana, sukari, mabati, saruji, mafuta na vitu vingine kwa kweli hali ni mbaya," amesema Mdude.

Naye aliyekuwa mgombea ubunge Musoma mjini, Julius Mwita amewaomba wakazi wa Musoma kukiunga mkono chama hicho ili kiiondoe CCM madarakani, kwani wameteseka kwa muda mrefu licha ya nchi kuwa na rasilimali nyingi ambazo zikitumika vema zinaweza kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla.

"Tunajua watu wa Musoma walishaikataa CCM kitambo sana na hata 2020 waliamua kukipigia kura za ushindi Chadema, lakini kwa vile tulikuwa hatujajiandaa kupambana tuliamua kupotezea ila mwaka 2025 tuko tayari kwa lolote," amesema.

Katika hatua nyingine,  polisi wakiongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Mara, Matthew Ntakije wameongoza maandamano hayo ya amani kutoka katika eneo la Bweri hadi katikati ya mji umbali wa takriban kilomita nane.

Askari polisi wakiwa wamevalia sare zao walichangamana na waandamanaji huku wengine wakiwa na kazi ya kuelekeza magari sehemu ya kupita, huku wengine wakiwaelekeza waandamanaji wapite wapi ili kujikinga na ajali.

Lissu ataka mapambano Katiba mpya

Kwa upande mwingine, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amewataka wananchi kujitokeza kupambana kupata Katiba mpya ili kujikomboa katika ugumu wa maisha.

Lissu aliyeongoza maandamano na baadaye kufanya mkutano katika mji wa Babati mkoani Manyara amesema umaskini wa wananchi unasababishwa na Katiba mbovu.

“Katiba ni utaratibu wa namna ya kuendesha maisha yako, usipoyajua yatakuumiza halafu utamlalamikia Mungu, usipokuwa na maarifa utaangamia,” amesema Lissu.

Amesema ugumu wa maisha unatokana na Katiba ambayo imempa rais mamlaka ya kufanya anachotaka.

 “Tumekuwa na Katiba ambayo imefanya nchi hii ni mali ya rais, ukiangalia wasimamizi wa uchaguzi majaji na tume inayosimamia vyote ni vya kwake,” amesema.

Lissu ambaye aliyewahi kuwa mbunge wa Singida Mashariki amesema, mtu hawezi kusema Katiba sio muhimu kwani nchi hii kwa mujibu wa sheria inasema ardhi mali ya umma chini ya udhamini wa Rais.

Amesema kama ni mali ya Rais anaweza kufanya lolote, kupitia miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hakuna sababu ya kushangilia.

 “Tunapaswa kuomboleza tukisema haituhusu wafanyabiashara mtakuwa mnawafanyia kazi wengine wananeemeka, tunataka Katiba mpya iondoe miaka 60 ya manyanyaso,” amesema.

Hata hivyo, Lissu amebainisha kuwa endapo kutakuwa na Katiba inayoweza kumshughulikia rais, na wakuu wa mikoa na wilaya hawataleta mchezo.

 “Tunataka Katiba mpya itakayoondoa kinga za viongozi, itakayorudisha bunge na wabunge ambao wanaungwa mkono na wananchi na Katiba itakayosema ardhi ni yetu wadhamini ni sisi wenyewe,”amesema na kuongeza.

 “Hakuna sababu ya kuwa na Katiba itakayosema mdhamini ni Rais, ili yote yawezekane tunahitaji nguvu kubwa sana, hawa watu wana fedha nyingi na wanazitumia kuhonga tusipokuwa waangalifu watatuvuruga na sisi,” amesema.

Amesisitiza kuwa ili kuwakabili inawabidi kuwa na nguvu kubwa hivyo, maandamano wanayofanya ni ya watu wenye manung’uniko, wanaoandamana ni wale wanaoumizwa.

 “Tuungane kwa pamoja tuna uchaguzi mwaka huu na mwaka ujao tusiwape nafasi tena kuanzia kwenye mitaa na vijiji, tafuteni watu wasiowageuka, pamoja na umaskini wetu na unyonge wetu tukiamua tunaweza,” amesema.

Mbali na Lissu, alikuwepo pia mwanasheria maarufu, Boniface Mwabukusi aliyewataka wananchi wa Babati kuiondoa CCM madarakani, akisema imeshindwa kuwaletea maendeleo.

Naye Katibu wa Kanda ya Kaskazini ya chama hicho, Aman Golugwa amesema wananchi wanaoandamana maeneo mbalimbali wakiwa na mabango ni wafanyabiashara, vijana kwa wazee wakihitaji haki zao.

Amesema Serikali inapaswa kutenda haki na wasiposikia wataendeleza maandamano bila kusitisha kwa kuwa Watanzania wanahitaji Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi.

 “Hatuhitaji uchaguzi kama uliofanyika mwaka 2019/2020 wagombea wetu walienguliwa bila sababu za msingi, wengi wao wakapita bila kupingwa safari hii hatutakubali,” amesema Golugwa.