Mbowe atinga kwa mabalozi, Lwaitama amvaa Wasira

Balozi wa uingereza nchini Tanzania , David Concar akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe walipokutana jijini Dar es salaam .Picha Mtandao

Dar/Unguja. Kutokana na kauli za Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Stephen Wasira za kukosoa mpango wa Chadema kuandaa maandamano Januari 24, mwaka huu, kupinga miswada ya sheria za uchaguzi, chama hicho kimemjibu kikitaka asome vizuri tamko la maandamano hayo.

Januari 13, 2024 Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe alitangaza vuguvugu la kudai haki litakaloambatana na maandamano ya amani kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kuhusu miswada mitatu.

Miswada hiyo ni wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili Januari 17, mwaka huu, Wasira pamoja na mambo mengine alihoji sababu ya Chadema kupanga kufanya maandamano kabla ya kusubiri Bunge kujadili maoni ya wadau na kupitisha sheria.

“Sasa mimi nauliza, Bunge halijamaliza kazi yake ya kuchakata maoni, litakutana mwezi ujao na Mbowe anaitisha maandamano Januari 24, siku chache kabla ya Bunge, halafu anasema maoni ya wananchi yamekataliwa, yamekataliwaje wakati hawajamaliza?” alihoji Wasira.

Akizungumzia kauli za Wasira, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Profesa Azaveli Lwaitama alisema kada huyo wa CCM hajaelewa lengo la chama hicho kuandamana.

“Mwenyekiti (Mbowe) ameeleza kuwa, jinsi kamati ilivyoyapokea mapendekezo ya Chadema kupitia wasilisho la Katibu Mkuu, John Mnyika ilionyesha mwelekeo wa kukataa mapendekezo yote matatu ya msingi ya Chadema,” alisema.

Alitaja mapendekezo hayo kuwa ni Chadema kutaka Bunge liiombe Serikali iitoe miswada hiyo mitatu bungeni na badala yake iletwe kwanza bungeni miswada miwili.

Alisema, “Pendekezo la pili la Chadema ni kuwa kwa sasa Serikali ipeleke bungeni kwanza muswada wa kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.”

“Huu ndiyo muswada utakaounda vyombo vya kimuafaka vya kusimamia kukamilishwa kwa Mchakato wa kuandika Katiba mpya,” alisema.

“Vyombo hivi ni kama vile jopo la wataalamu ambalo litapendekeza maudhui ya Katiba mpya ikiwa ni pamoja na vifungu pendekezwa kuhusu masuala ya uchaguzi, Tume ya Uchanguzi na usajili wa vyama vya siasa,” alisema.

Alisema suala la kuundwa kwa jopo la wataalamu ni pendekezo la kikosi kazi kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala.

“Chadema kimeafiki pendekezo hilo, lakini kimependekeza kuwepo pia Tume ya Maridhiano (reference group) na mkutano mkuu au Bunge la Katiba),” alisema.

Kuhusu pendekezo la tatu, alisema chama hicho kinaitaka Serikali ipeleke baadaye kidogo muswada wa kufanya mabadiliko madogo ya Katiba ya sasa kuhusu masuala ya uchaguzi, Tume ya Uchanguzi na usajili wa vyama vya siasa.

“Muswada huu wa pili kati ya miwili inayopendekezwa na Chadema iletwe bungeni baada ya kuanza kufanya kazi kwa vyombo vya kimuafaka vya kusimamia kuandikwa kwa Katiba mpya (hususani jopo la wataalamu).

“Hivyo ndivyo vitakuwa vyombo sahihi vya kujenga muafaka wa kitaifa kuhusu maudhui ya Katiba mpya pendekezwa ikiwa ni pamoja na masuala ya uchaguzi, Tume ya Uchanguzi, na usajili wa vyama vya siasa,” alisema.

Alisema mapendekezo hayo matatu ya msingi ya Chadema yalizuiwa kuwasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge kwa mdomo, badala yake ikamwelekeza Mnyika awasilishe yale ya kifungu kwa kifungu.

“Kwa kweli Kamati iliweka wazi kuwa hakuwa tayari kupokea mawazo ya wadau yaliyogusia kutanguliza mabadiliko madogo ya Katiba ya sasa kabla ya kuzungumzia maudhui ya miswada mitatu ilivyokuwa mbele ya Bunge, alisema Profesa Lwaitama na kuongeza:

“Maandamano ni njia sahihi ya kushinikiza Kamati ya Bunge kupendekeza kuwa Bunge litakalokaa mwezi ujao analolitaja Wasira liitake Serikali kuiondoa bungeni hii miswada mitatu. Maandamano baada ya Bunge kukaa yatakuwa hayana maana,” alisema.

Alisema msingi wa maandamo ni kuwa Bunge likikaa na Kamati ikawa haikupendekeza Serikali iiondoe miswada hii bungeni basi Serikali yenyewe iiondoe kwa kushinikiza na maandamano.

“Lengo la maandamano ni kushinikiza Serikali kuiondoa miswada hii na isipelekwe bungeni kujadiliwa, badala yake walau muda wa kikao cha Bunge utumiwe vizuri kujadili hatua mahususi za Serikali kukabili suala la ugumu wa maisha,” alisema.

Kwa upande wake, alipotafutwa jana alisema alichokizungumza Profesa Lwaitama ni hoja za Chadema na sio wananchi waliofika mbele ya Kamati ya Bunge.

“Viongozi na makada wa Chadema waliofika mbele ya kamati na wananchi wengine, hakuna aliyeleta hoja kama za Lwaitama na ndio sababu baadhi ya watu walio karibu nao wanapinga,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama, Jumatano wiki alieleza kushangazwa na kauli ya Chadema kudai hakikupewa nafasi ya kusikilizwa na kamati hiyo.

Alisema kati ya vyama vyote vya siasa, Chadema ndiyo ilikuwa na makundi mengi ya ndani ya chama yaliyowasilisha maoni yao.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni Bunge la Wananchi, Baraza la Vijana (Bavicha), Baraza la Wanawake (Bawacha) na chama chenye yaliyowasilishwa na Mnyika.

“Hakuna chama kilichopewa nafasi kama Chadema wote waliokuja katika kamati walipewa nafasi ya kusikilizwa. Niwaondoe hofu Watanzania maoni yote yatatendewa haki,” alisema.

Dk Mhagama alisema tayari kamati imeshawasilisha serikalini awamu ya kwanza ya rasimu ya uchambuzi wa sheria tatu za uchaguzi baada ya kupokea maoni kutoka kwa makundi mbalimbali.

Miswada hiyo ilifikishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10 mwaka jana, huku kamati ikisikiliza maoni ya wadau kwa siku tatu mfululizo kuanzia Januari 6, 2024.

Mhagama alisema maoni kutoka watu na taasisi 1,707 zikiwamo za kidini, asasi za kiraia 31 zilizowakilisha asasi nyingine 400, wachangiaji binafsi 68 na vyama 13 vya siasa walishiriki kutoa maoni.

Alisema maoni hayo yamegawanywa katika makundi matatu ambayo ni yanayohusiana na mabadiliko ya sheria zilizopelekwa bungeni, ambayo yanaendana na Katiba ya nchi.

Ametaja kundi jingine ni maoni ambayo utekelezaji wake utasababisha Katiba iliyopo hivi sasa kuvunjwa, na yale yanayohusu masuala ya kiutawala.

Alisema maoni yanayovunja Katiba hawawezi kwenda nayo bungeni bali yatasubiri mchakato wa Katiba mpya utakapokuja. Awamu ya kwanza ya uchambuzi iliyoambatanishwa na maoni ya kamati imerudishwa serikalini kwa ajili ya kupitiwa kabla ya kurejeshwa tena kwa kamati hiyo.


Chaumma watoa neno

Kwa upande wake, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kuzungumza nao kwa ajili ya kuleta muafaka wa kitaifa.

Katibu Mkuu wa Chaumma Taifa, Ali Omar Juma, alisema wanaamini mazungumzo yataliondoa Taifa katika sintofahamu zinazoendelea badala ya kukaa kimya na kuruhusu maandamano yanayopangwa kufanyika.

“Ili kuiondoa nchi katika sintofahamu basi haina budi Rais Samia kukubali ombi hili la kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kwani hili lipo chini ya mamlaka yake na katika kujenga, usione aibu kukosolewa ingawaje aliruhusu hilo,” alisema Ali.

Alisema kutoa uhuru wa mtu kuzungumza au maoni ni njia ya kujenga demokrasia kwa vyama vya siasa na kuvifanya kuwa na imani katika kuhakikisha yale wanayoyatoa yatafanyiwa kazi.

Hata hivyo, akizungumzia miswada ya sheria za uchaguzi, alisema inatakiwa kufanyiwa marekebisho na isiwe sababu ya kuligawa Taifa.