Bemba wa Congo aigeuzia kibao ICC, aidai fidia Sh176 bilioni kwa kumuweka mahabusu

Monday March 11 2019

 

Aliyekuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jean-Pierre Bemba anadai fidia ya euro 68 milioni (sawa na Sh176 bilioni za Kitanzania) katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) baada ya kuondolewa makosa ya kufanya uhalifu wa kivita mwaka jana, mwanasheria wake amesema.
Mwanasheria huyo alisema mali za Bemba -- ambazo ni pamoja na ndege saba na nyumba tatu za kifahari zilizoko Ureno -- ziliachiwa "zioze tu" na mahakama wakati akishikiliwa gerezani The Hague.
Juni mwaka jana, Bemba alionekana hana hatia ya makosa ya mauaji, kubaka na utekaji nyara, vitendo vilivyofanywa na askari wa kikosi chake binafsi katika nchi jirani ya Afrika ya Kati mwaka 2002-3. Hata hivyo, mahakama ilimuona kuwa na hatia ya kuhonga mashahidi.
"Mtu asiye na hatia alipoteza miaka kumi ya maisha yake," amesema mwanasheria huyo, Peter Haynes katika nyaraka zilizotumwa ICC.
"Lengo ni kujaribu kufidia baadhi ya madhara yaliyofanywa kwa mtu huyu na familia yake kutokana na kukamatwa, kukaa mahabusu na vitendo vingine vilivyofanywa na mahakama na wahusika wengine," ameongeza Haynes.
Bemba alirejea nchini kwake baada ya kuachiwa huru na mahakama hiyo lakini akazuiwa kushiriki uchaguzi wa Congo kutokana na kukutwa na hatia ya kutoa rushwa.
Madai hayo ya fidia yanaongeza mzigo wa matatizo kwa ICC, ambayo iliundwa mwaka 2002 kushughulikia makosa makubwa ya uhalifu wa kivita duniani lakini imekumbana na changamoto kadhaa, kama ya kuachiwa huru kwa Bemba na mwezi Januari, kiongozi wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo.
Haynes alisema madai ya euro 68 milioni ni madogo kuliko nusu ya bajeti ya mwaka ya mahakama ya ICC.
Lakini Haynes alisema Bemba alikuwa tayari kuchangia euro 22 milioni -- kama atafidiwa malipo yote -- "kwa ajili ya kufidia wananchi wa Afrika ya Kati".
Fedha hizo zitatokana na madai ya fidia kwa ajili "kupoteza miaka kumi ya maisha yake".
"Kwa miaka kumi mali za Bemba, ambazo ni pamoja na ndege saba, nyumba tatu za kifahari nchini Ureno na sehemu tatu za ardhi nchini Congo na boti mbili ziliachiwa tu zioze," anasema Haynes.
Alipoulizwa kuhusu nani atakayelipia fidia hiyo, Haynes alisema mteja wake anastahili fidia kama inavyoelezwa kwenye nyaraka za kuanzisha ICC, Katiba ya Rome.
"Nategemea, na nina uhakika walipa kodi watategemea watashughulia masuala ya bima kwa ajili ya suala hili. Si kosa la Bemba au langu kama hawafanyi kazi na kuweka bima kwa ajili makosa wanayoweza kufanya," aliongeza. AFP

Advertisement