Ethiopia ya kwanza Afrika kununua Boeing 737 MAX 8

Muktasari:

Ndege aina ya Boeing 737-Max 8 iliyopata ajali leo asubuhi ilikuwa ni ndege mpya, iliyokabidhiwa kwa shirika la ndege la Ethiopia Julai mwaka jana

Addis Ababa. Ndege ya Ethiopia iliyopata ajali na kuua abiria wote ni toleo jipya la Boeing 737 aina ya MAX 8, lililoifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza Afrika kununua aina hiyo ya ndege.

Ndege hiyo mpya ilianza kufanya kazi Novemba 2018 na zaidi ya mashirika tisa ya ndege duniani yanamiliki ndege hizo za familia ya MAX. Kuna MAX 7, MAX 8, MAX 9 na MAX 10.

Shirika la Ethiopia linatajwa kuwa moja ya mashirika bora zaidi ya ndege barani Afrika na linakadiriwa kuwa na ndege kubwa zaidi ya 90 huku likisafiri kwenye maeneo zaidi ya 100 duniani. MAX 8 ni toleo lilitoka mwaka 2013

Ndege aina ya Boeing 737-Max 8 iliyopata ajali leo asubuhi ilikuwa ni ndege mpya, iliyokabidhiwa kwa shirika la ndege la Ethiopia Julai mwaka jana.

Wakati ikipata ajali ndege hiyo iliyokuwa na abiria 149 na wafanyakazi wanane. Ilikuwa ikitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole Addis Ababa nchini Ethiopia kwenda uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi nchini Kenya.

Boeing imetoa tamko la mstari mmoja Jumapili, ikisema kuwa " Boeing ina taarifa za ajali hiyo ya ndege na inafuatilia kwa ukaribu kabisa."

Kampuni ya Flightradar inayofuatilia urukaji wa ndege kupitia akaunti yake ya Twitter imesema kuwa kasi ya kuruka ndege hiyo haikuwa ya kawaida kwani ilikuwa ya kuyumbayumba.

Boeing 737-MAX 8 inafanana na aina ya ndege iliyoruka Oktoba kutoka Jakarta na kuanguka katika Bahari ya Java baada ya dakika chache, na kuua watu wote 189 waliokuwa katika ndege hiyo ya Lion Air.

Mashirika mengine ya ndege duniani yanayomiliki familia ya MAX ni Norwegian Air, Air China, TUI, Air Canada, United Airlines, American Airlines, Turkish Airlines, Icelandair na FlyDubai.