Gavana Joho akataa siasa mwezi wa Ramadhani, awa mhubiri

Mombasa. Mwezi mtukufu wa Ramadhani umemgeuza Gavana wa Mombasa, Hassan Joho anayejulikana kwa ujasiri wake wa kisiasa na kupambana na yoyote kuwa mhubiri wa dini.

Joho ambaye ni maarufu wa kupambana na yeyote kwenye siasa ameonekana kuwa na mwenendo tofauti mbali na ule uliozoeleka katika ulingo wa siasa.

Anapoulizwa na wakazi maswala ya siasa alisema hatozungumzia swala hilo hadi amalize Ramadhani.

“Kuna wakati wa siasa na utakuja lakini sasa ni wakati wa Ramadhani ambapo tunamtumikia Mungu, ni mwezi wa mapenzi, kutoa sadaka, kusaidia wasiojiweza na kuombeana. Tutaongea kuhusu siasa wakati wake lakini mwezi huu Mtukufu huwa hata nazima simu yangu sababu sitaki kukosa baraka,” alisema.

Kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo, gavana huyo ameonekana kuwa mtulivu akitumia muda mwingi kuhubiri utangamano kati ya jamii zote nchini, umuhimu wa kuomba, kupendana na kufuata nguzo za dini ya Uislamu.

Ramadhani ni mwezi mtukufu katika kalenda ya Kiislamu ambapo jamii hiyo inatakiwa kumtumikia Mungu kwa kufunga na kuongeza kuomba mwezi mzima.

Wengi wanapomwona gavana huyo wanadhani anatazamia kuwa mhubiri kwani kila anapochukua kipaza sauti anahubiri amani, upendo na umoja kinyume na hulka yake ya kauli kali za siasa alizokuwa akizitoa.

“Lazima tuungane kama jamii, tuishi kwa amani, tuache chuki na tuanze kupendana. Uislamu unatueleza kuwa tuko sawa sote. Waislamu ni ndugu lakini kwa jamii zingine sote tuko sawa,” alisema Joho hivi majuzi alipokutana na viongozi wa dini.

Aliwataka Waislamu waishi maisha mema ili jamii zingine zipendezwe na Uislamu na kuvutiwa kwenye dini hiyo.

 “Tukiishi kwa chuki tutafanya wengine washangae kuhusu Uislamu lakini tukiishi kwa wema watapendezwa na dini yetu,” alisema.

Amekuwa akijumuika na wakazi, vijana na viongozi wa dini kauli yake ikiwa upendo, umoja na utangamano wa jamii zote.

Aliwataka Waislamu kusimama wima katika dini na wasiyumbishwe na mawimbi yoyote huku wakimwomba Mungu.

Ni mwezi wa Ramadhani ambapo Joho anakuwa ‘mtakatifu’ akiweka dini mbele kushinda chochote kile. Lakini, wale ambao wameona video za Joho akiongea kuhusu kunyenyekea na kumwomba Mungu mwezi huu wanamkejeli wakisema anaazimia kuwa mhubiri.

Gavana Joho alisema kwa lolote lile ni sharti binadamu amweke Mungu mbele ili afanikiwe akisisitiza kuwa uongozi una majukumu magumu.

“Lakini, tuwe na imani katika safari hii, muhimu ni kwamba tushirikiane, kuna nchi ambazo Waislamu ni wachache lakini wana ushawishi mkubwa serikalini kwa mfano Afrika Kusini, humu nchini tunaweza kupata ushindi lakini lazima tujipange,” alisisitiza.

Pia, aliwataka Waislamu wasameheane ili wapate baraka kutoka kwa Mungu.