Jela miaka mitatu kwa kumuua kaka yake

Rukia Ally (24) akiwa mahakamani ambaye amefungwa miaka mitatu jela baada ya Mahakama kuu ya Tanzania kumkuta na hagia ya kuua bila kukusudia.Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania imemuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela,  Rukia Ally baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kaka yake, Said Ally bila kukusudia

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imemuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela,  Rukia Ally (24) baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kaka yake, Said Ally bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Julai 11, 2019 na msajili wa mahakama hiyo, Pamela Mazengo baada mshtakiwa kukiri kosa la kumuua Said bila ya kukusudia.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Mwasiti Ally alipomsomea mshtakiwa huyo kosa lake alikiri na kudai kuwa Rukia na Said ni ndugu na walikuwa wakiishi na wazazi wao eneo la  Mivumoni Madale.

Mwasiti amedai kuwa siku ya tukio muda wa jioni, Said alirejea nyumbani na kumkuta Rukia aliyekuwa ameondoka nyumbani hapo siku tatu zilizopita na kumfuata chumbani kumhoji alikokuwa.

Amesema Rukia alipoulizwa na kaka yake hakujibu chochote na Said kuanza kumchapa fimbo kwenye miguu.

Amesema wakati Said akifanya kitendo hicho alikuwa na kisu, Rukia alimpokonya bahati mbaya kikamchoma kaka yake kifuani upande wa kushoto, kuangua chini huku akitoka damu nyingi.

Hakimu Mazengo amesema baada ya mshtakiwa kukiri kosa hilo, mahakama imeona ana hatia ya kuua.

Kwa upande wake wakili wa utetezi,  Musa Mhagama aliiomba mahakama hiyo itumie kifungu cha 38 kifungo kidogo cha kwanza cha sheria kanuni ya adhabu sura ya 16 ya mwaka 2002.

"Namna kosa lilivyotendeka mshtakiwa aliweza kutenda kosa baada ya marehemu kushika kisu lakini wakati huo wote wawili hawakuwa na mahusiano mazuri," amedai  Mhagama.