Kiongozi upinzani akubali kushindwa Australia

Muktasari:

  • Kiongozi huyo amempigia simu mpinzani wake na kumpongeza kwa ushindi lakini pia aliueleza umati wa mashabiki wake kuhusu kushindwa huko

Melbourne, Australia. Kiongozi wa upinzani wa Chama cha Labor nchini Australia, Bill Shorten amempigia simu Waziri Mkuu, Scott Morrison kumpongeza kwa ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumamosi Mei 18, 2019.

Katika hotuba yake ya kukubali kushindwa Jumamosi usiku, Shorten aliueleza umati wa wafuasi wake kuwa inaonekana wazi kuwa Labor haitaweza kuunda Serikali inayofuata.

Akizungumza kutoka Melbourne, kiongozi huyo wa upinzani, alisema amempigia simu Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison kumpongeza kwa ushindi.

Aliongeza kuwa hatawania tena uongozi wa chama cha Labor katika uchaguzi unaofuata lakini akawataka wafuasi wake kuendelea na mapambano.

Baada ya kupokea simu hiyo, Waziri Mkuu Morrison ametanga kushinda tena nafasi hiyo katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali, akiuelezea ushindi huo kama muujiza.

“Siku zote naamini katika miujiza…na usiku wa leo tumetoa muujiza mwingine,” Morrison alilieleza kundi la mashabiki wake lililokuwa linashangilia.

“Usiku huu si kwa ajili yangu mimi, wala si kwa chama cha Liberal. Usiku huu ni kwa kila raia wa Australia anayetegemea Serikali yake imhudumie,” alisema Morrison akinukuliwa na Aljazeera.

Mapema, siku tatu kabla ya uchaguzi kura za maoni zilionyesha chama cha upinzani kingeweza kupata ushindi mwembemba dhidi ya Morrison.

Ingawa chama cha Morrison kimepata viti vingi katika Bunge la Wawakilishi kuliko Labor, haijafahamika kama kitaweza kupata wingi wa viti 76 vinavyohitajika kuunda Serikali, au la kitahitaji kuzungumza na wabunge wa kujitegemea kupata wingi wa kutosha.

Matokeo ya awali ya Tume ya Uchaguzi ya Australia yalionyesha chama tawala kikishinda viti 67 dhidi ya 55 vya Labor. Matokeo kamili yatatangazwa baadaye.

Australia imepata mabadiliko ya mawaziri wakuu mara sita katika miaka 12 iliyopita, mengi yakitokana na misuguano ndani ya vyama.

Shorten amekuwa anakinadi chama cha Labor kama fursa ya kuondokana na migogoro inayosababisha chama tawala kubadili mawaziri wakuu.