Meneja wa hoteli iliyoshambuliwa auawa akitoa huduma Kenya

Saturday January 19 2019

 

Nairobi,Kenya. Polisi nchini Kenya wamewafikisha watu watano mahakamani wanaohisi wamehusika na shambulizi la kigaidi lililofanyika wiki hii katika hoteli ya kifahari ya DusitD2 mjini Nairobi, ambapo watu 21 waliuawa.

Washambuliaji wote sita waliovamia hoteli hiyo na majengo yaliyokuwa karibu na hapo waliuawa, maofisa walisema huku msako wa kuwatafuta wale waliowasaidia kupanga shambulio hilo ukiendelea.

Kundi la al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia lilikiri kuhusika na shambulizi hilo.

Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema kuwa watu wote waliokuwa hawajulikani waliko wamepatikana.

Meneja DusitD2 auawa

Bernadette Konjalo aliyekuwa akifanya kazi kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano ya DusitD2 iliyopo Nairobi ambayo ilivamiwa na magaidi wiki hii ni miongoni mwa watu 21 waliopoteza maisha.

Meneja huyo ambaye alifanya kazi kwenye hoteli hiyo kwa miaka 10 aliuawa akiwa anawakaribisha wageni kwenye hoteli hiyo.

Dada wa meneja huyo, Camillus alisema kwamba alisikia taarifa za kifo cha mdogo wake kupitia kwa rafiki yake na aliamini kifo hicho baada ya kujaribu kumpigia simu yake huku ikiwa haipatikani.

Alisema awali alipata taarifa kuwa miongoni mwa watu walionusurika na kifo ni pamoja na ndugu yao huyo lakini ghafla taarifa zingine zikaja kwamba alipoteza maisha kwa kupigwa risasi.

Mke wa mtuhumiwa

Kumekuwa na taarifa za kukinzana kuhusu mwanamke anayetuhumiwa kuwa mke wa mojawapo wa watuhumiwa wa shambulio hilo, anayearifiwa kuwa alikamatwa Kiambu Kaskazini mwa mji mkuu wa Nairobi.

Polisi inasema haiwezi kuthibitisha au kupinga kwamba kuna aliyekamatwa.

“Hatutaweza kuzungumzia upelelezi wakati huu, kwa mfano tukizungumza kuhusu Kerubo wale waliokuwa karibu naye watasikia tumetangaza kuwa tunamtafuta, tunafanya nini...watatoroka’’, alisema msemaji wa polisi Charlse Owino.

Aliongeza kuwa cha msingi ni kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na kupanga na kutekeleza shambulia hilo wanakamatwa.

Advertisement