Mwanamke afariki akipendezeshwa matiti Kenya

Muktasari:

  • Upande wa watetezi wa hospitali hiyo ulikuwa ukiongozwa na Profesa Stanley Khainga, Dk Martin Ajujo na Dk Evans Cherono ambao walifika mahakamani kuelekeza utetezi wao dhidi ya jopo la uchunguzi la Bodi ya Madaktari na Bodi ya Meno Kenya (KMPDB)  kuhusu kifo cha Wanza

Nairobi, Kenya. Mwanamke aliyefahamika kwa jina la June Wanza (35) amefariki dunia baada ya kufanyiwa operesheni ya kuongeza matiti ambayo lengo lake lilikuwa ni kumpendezesha.

Mwanamke huyo mwenye watoto watatu alipoteza maisha siku mbili baada ya kumalizika kwa upasuaji huo.

Tukio hilo lilitokea Juni mwaka jana ambapo hospitali iliyohusika na operesheni hiyo ilikanusha ikidai haihusiki na tuhuma za kifo cha mwanamke huyo.

Katika kesi iliyofikishwa mahakamani jijini Nairobi leo, inaelezwa kwamba June Wanza alianza kuugua baada ya kufanyiwa upasuaji wa matiti kwenye Hospitali ya Surgeoderm Healthcare.

“Naweza kuthibisha kuwa mgonjwa aliyefariki dunia katika Hospitali ya Nairobi, aliletwa kutokana na matatizo aliyokumbana nayo huko alikokuwepo, alipitia mikononi mwa madaktari watatu,” alisema Dk Christopher Abeid.

Akizungumza mahakamani Dk Abeid alisema kwamba Dk Ajujo, alikuwa kwenye mafunzo ya awali ya udaktari.

Inavyofahamika ni kwamba Dk Ajujo na Profesa Khainga wana hisa kubwa kwenye hospitali hiyo ya Surgeoderm Healthcare Limited.

‘’Pia daktari Evans Charana, siyo miongoni mwa madaktari wenye leseni KMPDB,’’ alisema.