Obasanjo:Buhari anasuka mpango wa kuiba kura

Muktasari:

  • Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo  amesema kwamba Rais Muhammadu Buhari ameshaajiri maofisa usalama, na wa tume wapya ili kufanikisha uibaji wa kura kwenye uchaguzi Mkuu

Lagos, Nigeria. Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo amesema rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari, anayewania kiti cha urais kwa muhula wa pili, anaandaa mpango  wa kuiba kura ili aweze kushinda Uchaguzi Mkuu utakaofanyika  Februari 16 mwaka huu.

Obasanjo, ambaye alimuunga mkono Rais huyo wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 kwa asilimia mia moja  katika miezi ya hivi karibuni ameendelea kukosoa sera yake, na wakati huu anamuunga mkono mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa urais, Atiku Abubakar .

"Binafsi, nina wasiwasi kuhusu uadilifu, uhuru wa INEC (Tume ya Uchaguzi) kwa kuandaa uchaguzi wa haki, ulio huru na wa kuaminika," amesema Obasanjo katika barua iliyowekwa wazi.

Pia amemshtumu moja kwa moja Rais Buhari kwamba ameanza  kuajiri maofisa maalum  ili kuchakachua matokeo ya uchaguzi kabla ya uchaguzi.

"Watu wake wanafanya kazi usiku na mchana na maofisa wa usalama pamoja na wa Tume ya  Uchaguzi ili kukamilisha mpango wao kwa kuhesabu matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, uchaguzi wa magavana wa mikoa na uchaguzi wa urais kwa kumpa ushindi, " amesema Obasanjo

Obasanjo amemfananidha Rais Buhari na dikteta wa zamani wa nchi hiyo Sani Abacha, ambaye alitawala Nigeria tangu mwaka 1993 hadi 1998, akisema kuwa alikuwa tayari kufanya kilicho chini ya uwezo wake ili aendelee kubaki  madarakani.

Rais Buhari alisema kwamba ana uhakika wa ushindi kwenye kinyang’anyiro hicho kwa sababu amefanya mambo mengi ikiwamo kukuza uchumi wan chi hiyo kwa kiasi kikubwa tangu aingine madarakani 2015