Polisi wakabiliana na waandamanaji Hong Kong

Muktasari:

  • Maandamano hayo yalianza mapema mwezi uliopita kupinga mswada wa kuwahamisha wafungwa wa Hong Kong kushtakiwa upande wa China bara.

Hong Kong, China. Polisi mjini Hong Kong imefyatua mabomu ya machozi pamoja na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamefunga barabara.

Kwa siku mbili mfululizo waandamanaji mjini Hong Kong wamekuwa wakikabiliana na polisi.

Maandamano hayo yalianza mapema mwezi uliopita kupinga mswada wa kuwahamisha wafungwa wa Hong Kong kushtakiwa upande wa China bara.

Hata hivyo, licha ya mswada huo kufutwa, waandamanaji sasa wameingia mitaani wakishinikisha kuwapo kwa demokrasia kamili.

Katika hatua nyingine, Serikali nchini China imelaani machafuko hayo yanayoendelea katika visiwa hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa ofisi inayoshughulikia masuala ya Hong Kong na Macao, Yang Guang alisema maandamano hayo yamesababisha uharibifu mkubwa.

Yang Guang alisema maandamano hayo yamevuruga utulivu, utawala wa sheria, uchumi na maisha ya watu wa mji huo wenye utawala wa ndani.

Yang alisema Serikali kuu mjini Beijing inamuunga mkono kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam na polisi wa mji huo kwa hatua zinazochukuliwa kukabiliana na kile alichokiita matendo ya vurugu na yasiyozingatia sheria.

“Serikali ya China inatambua changamoto za Hong Kong na kwamba lazima itafute njia bora zaidi za kutatua wasiwasi wa vijana kuhusu makazi, ajira na masuala mengine,” alisisitiza Guang.