R Kelly sasa ana Sh29,000 kwenye akaunti

Wednesday April 17 2019

 

Chicago. Ukisikia siku ya kufa nyani miti yote huteleza, basi ndiyo haya yanayomkuta mwanamuziki R Kelly.

Mwanamuziki huyo anayepitia kipindi kigumu akikabiliwa na kesi ya unyanyasaji wa kingono, amejikuta akibaki bila salio baada ya mdeni wake kukomba Dola 154,527 za Marekani zilizokuwa katika akaunti yake.

Mtandao wa The Blast unaripoti kuwa unayo taarifa ya akaunti ya benki ya mwanamuziki huyo ambaye ametumiwa nakala akielezwa fedha zake kuchukuliwa na mdeni.

Inaelezwa kuwa aliyewahi kuwa mwenye nyumba wa R Kelly, alifungua madai baada ya kutolipwa limbikizo la kodi na mwanamuziki huyo.

Hukumu iliyotolewa iliagiza mwanamuziki huyo akatwe stahiki zake katika malipo ya kazi zake za muziki au zichukuliwe fedha zilizopo katika akaunti yake.

Pamoja na benki hiyo ya Wintrust kutoa fedha zote zilizopo na kubakiza Dola 13 ambazo ni wastani wa Sh29,000, bado hajafanikiwa kulipa deni lote.

Advertisement

Mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na nyimbo I Believe I Can Fly, The World’s Greatest, Sound of Victory na nyingine anadaiwa Dola 194,000 za pango la nyumba.

Mbali na kukabiliwa na kesi na madeni hayo, R Kelly pia amefunguliwa mashtaka kwa kushindwa kutoa fedha za matunzo kwa mzazi mwezake.

Chama cha waandishi, watayarishaji na wachapishaji wa muziki nchini Marekani  (Ascap), kimesema hakina fedha za kuwalipa kwa sababu mwanamuziki huyo hawadai.

Tumaini pekee la mdai huyo ni Kampuni ya Sony ambayo ameiandikia kumalizia takriban Dola 50,000 zilizosalia katika deni hilo.

Mwishoni mwa mwaka jana, wanawake zaidi ya watano wamejitokeza wakidai kutumikishwa kingono na mwanamuziki huyo.

Miezi miwili iliyopita alifunguliwa mashtaka 10 ya kuwanyanyasa kingono mabinti wa kati ya miaka 13 na 17 na iwapo atapatikana na hatia huenda akafungwa miaka 70.

Mwaka 2008, mahakama nchini Marekani ilimwachia huru katika madai ya kumshirikisha binti mdogo kucheza sinema ya ngono.

Jaji aliyetoa hukumu alisema mahakama inamwachia huru kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa mwanamke anayeonekana kwenye video hiyo ana umri mdogo.

Advertisement