Tshisekedi amteua Ilunkamba waziri mkuu DRC

Rais Felix Tshisekedi amemteua Profesa Sylvestre Ilunga Ilunkamba kuwa waziri mkuu mpya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Uteuzi huo umefanyika muda mfupi uliopita baada ya hapo awali waziri mkuu aliyekuwapo, Bruno Tshibala, kujiuzulu, kwa mujibu wa BBC

Sylvestre amewahi kushikilia nyadhifa tofuati serikalini.

Yeye ni mfuasi wa chama cha rais wa zamani nchini Congo, Joseph Kabila – PPRD kwa kuwa ndicho chenye wabunge wengi na kinastahili kutoa waziri mkuu.

Raia wa Congo wamesubiri zaidi ya miezi mitatu, bila kuwa na waziri mkuu wala kuunda baraza la mawaziri.

Mwanasisia huyu mwenye umri wa miaka 78 ambaye pia ni miongoni mwa viongozi wa chama cha Joseph Kabila, alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya Reli nchini Congo.

Aliwahi kutumika chini ya utawala wa Mobutu Seseko kama mshauri wake wa maswali ya uchumi.

Moise Katumbi arejea DRC

Mapema leo Mei 20, Kiongozi wa upinzani wa DRC, Moise Katumbi amelakiwa na maelfu ya wafuasi Lubumbashi baada ya kuishi uhamishoni kwa takriban miaka mitatu.

Katumbi, mmiliki wa michezo wa TP Mazembe amepokewa na maelfu ya wafuasi waliojawa na furaha na shangwe katika uwanja wa ndege wa Luano nchini Congo.

Kiongozi huyo wa upinzani amekuwa akiishi uhamishoni kwa miaka zaidi ya miwili iliyopita baada ya kushtakiwa na serikali ya rais wa zamani Joseph Kabila kwa makosa kadhaa ya uhalifu ukiwemo udanganyifu, kuwajiri mamluki na kujipatia uraia wa pili kinyume cha sheria.

Umati ulionekana ukimsindikiza Katumbi kuelekea katika uwanja wa michezo wa TP Mazembe.

Katika mahojiano na televisheni ya France 24, Katumbi alisema anapanga kurudi nyumbani Mei 20 ikiwa ni takriban miaka mitatu tangu aondoke nchini.

"Ni hakika kwamba Mei 20, nitakuwa Lubumbashi," Katumbi amenukuliwa na katika mahojiano hayo yaliofanyika Mei 6.

Alieleza kwamba baada ya kurudi Lubumbashi anapanga ziara ya kitaifa katika alichotaja kuwa ni 'kuwaliwaza' raia wa DR Congo, hususan "familia zilizoteswa... na walioishi katika tabu".

Mnamo 2016, Moise Katumbi, alihukumiwa kifungo cha miaka 3 jela kwa kununua nyumba kinyume cha sheria kwenye mji ulio mashariki mwa nchi wa Lubumbashi na pia kutuhumiwa kwa kuwaajiri mamluki wa kigeni ili kupanga njama dhidi ya serikali.

Wakati wa kuapishwa kwake, Rais Tshisekedi, aliahidi kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa, walio uhamishoni na watu wote waliofungwa wakati wa maandamano yaliyofanyika kabla ya uchaguzi wa mkuu.