Watu mashuhuri waliopoteza maisha ajali ya ndege Ethiopia

Muktasari:

  • Ni baadhi ya viongozi wa sekta mbalimbali ambao wamepoteza maisha kutokana na ajali ya ndege iliyotokea jana Ethiopia

Mashirika. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetoa taarifa rasmi kuhusu kufariki kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Kenya na Ofisa Mkuu wa Soka Kenya, Hussein Swaleh Mtetu ambaye alikuwa miongoni mwa Wakenya 32 waliofariki.

Taarifa zinasema Swaleh alikuwa anarudi nyumbani baada ya kumaliza kazi yake akiwa kamishna katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Ismaily na TP Mazembe.

Mchezo uliohudhuriwa na kiongozi huyo ulizikutanisha timu hizo za mataifa ya Misri (Ismaily) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Mazembe) ulichezwa Ijumaa mjini Alexandria.

Naye Mkuu wa Itifaki wa Somalia ameripotiwa kuwa mmoja wa watu waliokufa kwenye ajali hiyo, kwa mujibu wa Kituo cha Redio cha Dalsan, kinachomilikiwa na redio ya Somalia.

Nalo, Shirika la Umoja wa Mataifa Unesco limeelezea masikitiko kwa kumpoteza mwanaharakati anayetetea uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa waandishi wa habari Kenya, Anthony Ngare aliyehudumu katika kitengo cha tume ya kitaifa Kenya kwa Unesco.

Kwa waliokuwa karibu naye wanamkumbuka kwa jinsi alivyokuwa shabiki wa Arsenal ya England.