Wiki muhimu kwa Rais Trump kuhusu ujenzi ukuta wa Mexico

Ijumaa ya wiki hii itakuwa siku muhimu kwa Rais Donald Trump wa Marekani kuona kama mkakati na ahadi yake ya kujenga ukuta katika mpaka wa nchi yake na Mexico inatimia au la.

Siku hiyo ndiyo itakuwa tamati ya muda wa mazungumzo uliotolewa kwa pande mbili zinazovutana ndani ya vikao vya Baraza la Congress na lile la Wawakilishi kufikia mwafaka wa kuidhinisha fedha zinazohitajiwa na Trump kutekeleza ujenzi wa ukuta huo.

Pande mbili hizo ni ule wa chama cha Republican wanaomuunga mkono Trump kutekeleza mkakati huo na Democrats unaompinga, Jumatatu walifikia makubaliano yenye masharti ambayo hata hivyo hayajawekwa wazi kuhusiana na suala la ulinzi wa mpaka kwa lengo la kuidhinisha fedha zilizoombwa na Serikali ili kuepusha kufungwa tena kwa shughuli za kiofisi za wizara na idara mbalimbali kama ilivyokuwa Desemba mwaka jana.

Wajumbe wa majadiliano hayo wamekubaliana kuepusha kufungwa kwa shughuli za Serikali na kuridhia kupitisha Dola 1.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vizuizi vipya katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Hata hivyo, makubaliano hayo yanapaswa kuidhinishwa na Baraza la Congress na Rais Trump mwenyewe kabla ya kuingizwa katika utekelezaji.

Desemba mwaka jana ofisi mbalimbali za umma zilisimamisha huduma baada ya baraza hilo kutoidhinisha bajeti kupinga maombi ya Dola 5.7 zilizoombwa na Serikali ya Marekani kwa ajili ya kujenga ukuta huo.

Makubaliano hayo yaliyofanyika katika kikao cha ndani jijini Washingiton, Jumatatu, yanaashiria kuwa huenda sasa pande mbili hizo zikafikia mwafaka na kunusuru mkwamo mwingine wa shughuli za kiofisi baada ya ule wa awali uliosababisha hasara ya Dola 11 bilioni katika uchumi wa Marekani.

Seneta kutoka chama tawala cha Republican cha Rais Trump, Richard Shelby, akizungumza baada ya mazungumzo ya wiki hii, alisema mambo yote muhimu waliyokuwa wakitofautiana yamepatiwa mwafaka “tumefikia makubaliano katika mambo yote muhimu. Watendaji wetu wanayaweka pamoja, tunaamini kama yatapitishwa yatafungua milango kwa Serikali”.

Mazungumzo hayo awali yaligonga mwamba baada ya wajumbe kutoka chama cha Democrats kutaka ukomo wa wahamiaji ambao hawajasajiliwa kisheria waliopo nchini humo na ambao wanaweza kupewa hifadhi katika kambi maalumu.

Hatua hiyo inaelezwa kufikiwa baada ya Democrats kuridhia baadhi ya mapendekezo ya Serikali huku wakitaka vitanda vilivyoko katika kambi hizo vipunguzwe kutoka 49,057 hadi 40,250.

Kwa nini Trump anang’ang’ana na ukuta

Trump aliyeingia Ikulu kwa tiketi ya Republican, alikutana na viongozi wa Democratic bungeni, Nancy Pelosi ambaye ni Spika wa Baraza la Wawakilishi na Chuck Schumer, kiongozi wa wabunge wa Democratic katika baraza la Seneti, lakini mazungumzo yao yalishindwa kupata mwafaka.

Ujenzi wa ukuta huo ni moja ya ahadi za Trump alizozitoa wakati wa kampeni zake alipokuwa akiwania kiti hicho mwaka 2016.

Pelosi alikosoa uamuzi wa kufunga shughuli za Serikali uliofanywa na Trump kisa kutoidhinishwa kwa feha za ukuta na kusema hakupaswa kufanya hivyo.

Rais Trump mwenyewe akihutubia umati wa watu katika mji wa El Paso, uliopo mpakani mwa Marekani na Mexico, hivi karibuni alisema hajapata muda wa kupitia makubaliano yaliyofikiwa wiki hii, lakini alisisitiza kuwa hatasaini mapendekezo yatakayoruhusu kuingia nchini humo watu hatari, watakaosababisha vurugu.

Trump alisisitiza kujengwa kwa uzio utakaozitenganisha nchi hizo kama mkakati wa kiulinzi na usalama kujilinda dhidi ya watu hatari kwa nchi hiyo.

Rais huyo amewahi kutishia kutumia njia mbadala kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta huo ikiwamo kutangaza hali ya dharura itakayompa uhalali wa kutumia fedha kutoka kwenye fungu la wizara ya ulinzi kufanikisha mkakati wake. Trump anahitaji bajeti ya dola bilioni 5.7 kufanikisha ujenzi wa ukuta huo akiamini utasaidia kupambana na wimbi la wahamiaji wanaoingia Marekani kinyume cha sheria kupitia Mexico.

Anasema hali katika mpaka huo inazidi kuwa mbaya kiasi cha kugeuka mzozo wa kibinadamu.

Anasisitiza kuwa kushindwa kuwadhibiti wahamiaji haramu kunaumiza mamilioni ya Wamarekani huku mzozo wa kibinadamu na kiusalama ukiongezeka katika mpaka huo.

Kwa mujibu wa Trump, wahamiaji haramu ndio chanzo kikubwa cha uhalifu na uingizwaji wa dawa za kulevya nchini humo mambo yanayompa nguvu ya kuendelea kuitetea hoja ya ukuta.

‘’Kwa miaka mingi maelfu ya Wamarekani wameuawa kikatili na watu walioingia kinyume cha sheria nchini mwetu na maelfu ya watu watapotea tusipochukua hatua sasa. Huu ni mzozo wa kibinadamu. Hivi karibuni watoto wahamiaji 20,000 waliletwa Marekani kinyume cha sheria, hilo ni ongezeko kubwa. Watoto hawa wanatumiwa na makundi katili ya kihalifu,’’ anasema Trump.

Baada ya kushindwa kufanikiwa kwa mazungumzo ya awali, Rais Trump alisema: “Hatuna chaguo lingine zaidi ya kujenga ukuta imara”. Aliongeza kuwa, “kama tukishindwa kufikia makubaliano yenye tija katika Bunge la Kongresi, basi shughuli za Serikali zatasitishwa Februari 15 au nitatumia mamlaka niliyopewa chini ya sheria na Katiba ya Marekani kukabiliana na dharura hiyo.

Hata hivyo, Spika Pelosi alimshutumu Trump kuishikilia ‘mateka’ Serikali ya Marekani na kutengeneza mzozo katika mpaka huo.

Mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kijasusi ya Baraza la Wawakilishi, Adam Schiff amlimshutumu Trump akisema katika historia ya Marekani, marais wameitumia Ikulu ya nchi hiyo kuiunganisha nchi, lakini kwake imekuwa tofauti akidai amekuwa akiitumia kuchochea hofu na mgawanyiko.

Wakati mgogoro huo ukipita katika hatua mbalimbali, uchunguzi uliofanywa na mashirika ya Harvard CAPS na Harris, umebaini kuwa asilimia 66 ya Wamarekani wanapinga kujengwa kwa ukuta huo. Ripoti ya uchunguzi huo inaonyesha asilimia 31 ya Wamarekani wanasema ujenzi wa ukuta sio jambo la dharura na kwamba utagharimu fedha nyingi huku asilimia 31 nyingine wakishauri kutumika njia bora zaidi kwa ajili ya usalama wa mpakani.