Dk Bashiru amuonya waziri wa Viwanda nchini Tanzania

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema Waziri wa Viwanda, Innocent Bashungwa atatumbuliwa ikiwa atashindwa kutimiza azma ya Serikali ya kufufua viwanda

Moshi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema Waziri wa Viwanda, Innocent Bashungwa atatumbuliwa ikiwa atashindwa kutimiza azma ya Serikali ya kufufua viwanda.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 9, 2019 baada ya kutembelea kiwanda cha kukoboa kahawa cha TCCCO kilichopo manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kufufua viwanda na kwamba jambo linalopaswa kufanya ni kujiandaa katika masuala ya ushirika, ubunifu na ujuzi ili nchi iweze kujisimamia.

“Nimesoma katika kitabu cha wageni  waziri wa Viwanda alikuwa hapa Mei 28 (aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda) na ameshatumbuliwa, na huyu aliyepo ajiandae kutumbuliwa maana kama tunasema tunahitaji uchumi wa viwanda halafu havifufuki.”

“Barabara zinajengwa unaziona, SGR (Reli ya kisasa) unaiona, kwa nini hatuoni viwanda vinafufuliwa?” amehoji Dk Bashiru.

Amesema kuendesha kiwanda kama TCCCO ni lazima kuwepo na kiwanda cha magunia, “Bado kuna kazi kubwa katika vita ya uchumi, kiwanda hiki ambacho kilitarajiwa kuwa na wafanyakazi zaidi ya 4000 leo kinao 44, mitambo inaitwa mipya lakini haifanyi kazi na imenunuliwa kwa kuuza mali za kampuni, hizi ni hujuma.”

Amebainisha kuwa viwanda vyote vilivyoanzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza vina hali mbaya.

Awali akisoma taarifa ya TCCCO, makamu mwenyekiti wa bodi ya kiwanda hicho, Kandata Kimaro amesema kinadaiwa Sh1.2 bilioni na kwamba kahawa inayopokewa kiwandani imeshuka kutoka tani 31,000 mwaka 1988/1989 hadi  tani 912 msimu wa mwaka 2018/2019.