Gesi mbioni kufuta matumizi ya mkaa

Thursday February 14 2019

Mkurugenzi wa Masoko wa ORYX, Mohammed Mohammed

Mkurugenzi wa Masoko wa ORYX, Mohammed Mohammed akizungumza katika mjadala wa Jukwaa la Frika lililojadili matumizi ya mkaa, uchumi na mazingira yetu, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Taifa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira, Ally Mufuruki Picha na Said Khamis 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa misitu kutokana na matumizi ya mkaa na kuni kwenye Jukwaa la Fikra la Mwananchi lililofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam ni matumizi ya nishati ya gesi.

Katika jukwaa hilo la tatu ambalo liliwakutanisha wadau wa sekta ya mazingira na nishati nchini kupitia kujadili mada ya “Mkaa, Uchumi na Mazingira yetu,” walizungumzia matumizi ya gesi, nishati ambayo baadhi ya wananchi wamekuwa wakiiona aghali na hatari kwa usalama wao.

Katika mjadala, hoja ya kupunguza matumizi ya mkaa ndiyo iliyotalawa sambamba na mapendekezo ya njia za kisayansi ili ushawishi wa matumizi ya gesi ili kuepuka athari za kiafya, kiuchumi na kijamii katika mkaa.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya gesi ya Oryx, Mohammed Mohammed ndiye aliyechokoza mada kuhusu umuhimu wa kugeukia matumizi ya gesi zaidi. Akitumia takwimu alisema Tanzania inaweza kuachana na matumizi ya mkaa miaka ijayo.

Alisema gesi inayotumika majumbani za kwenye mitungi yaani (Liquiefied Petroleum Gas – LPG) ni nishati inayopika kwa ufanisi zaidi kuliko nyingine za asilia na matumizi yake yamekuwa yakiongezeka nchini mwaka hadi mwaka.

“Mwaka jana tani 150,000 zilingizwa, kati ya hizo 80,000 zilitumika nchini na nyingine kuuzwa nchi jirani. Sasa tani 80,000 za mwaka jana ukilinganisha na tani 4,500 zilizotumika mwaka 2006 ni sawa na ongezeko la mara 17,” alisema.

Aidha, alisema uwezo wa kuhifadhi wa LPG umeongezeka kutoka tani 1,300 mwaka 2006 hadi kufikia tani 13,000 kwa mwaka jana huku matarajio ya mwaka huu yakiwa kufikia uwezo wa kuhifadhi wastani wa tani 17,000, sawa na ongezeko la mara 14.

Alisema takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa matumizi ya nishati hiyo majumbani akitoa mfano wa mwaka 2006 ambako ni asilimia 2.7 ya kaya 100 ndizo zilitumia gesi ya kupikia lakini mwaka jana, idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia asilimia 10 ya kila kaya 100.

Ingawa ukuaji huo wa matumizi ya gesi ni mzuri alisema bado ni mdogo ikilinganishwa na nchi kama Brazil ambayo imefikia asilimia 90 ya matumizi ya LPG na Indonesia asilimia 75.

“Kwa hiyo tunaona nafasi ni kubwa kwa Tanzania kufikia viwango vya juu vya matumizi ya gesi,” alisema.

Mohammed alisema kutokana na kiwango hicho cha matumizi ya gesi, Taifa limefaanikiwa kuhifadhi mazingira na afya za watumiaji.

“Sasa wanasema mkaa ni rahisi lakini ukitazama katika matumizi halisi, nishati ya LPG ni rahisi sana kwa sababu Mtanzania wa kipato cha chini atalazimika kuwa na Sh1,500 hadi Sh3,000 kwa siku ili kupika mlo wake kwa mkaa lakini kwa mtumiaji wa LPG anatumia wastani wa Sh600 tu kupikia mlo uleule,” alisema Mohammed.

Changamoto ya kodi

Pamoja na urahisi wa bei anaoutaja Mohammed, changamoto kubwa ipo katika gharama za awali ambazo ni ununuzi ya mtungi, gesi yenyewe na viunganishi vyake ambavyo hugharimu kati ya Sh50,000 hadi Sh120,000 kutegemea na ukubwa wa mtungi ikilinganishwa na Sh7,000 kwa anayetumia mkaa.

“Tunashukuru Serikali iliondoa kodi ya gesi yenyewe (LPG) mwaka 2006, ikaondoa kodi kwenye mtungi wa gesi lakini bado kuna kodi ya VAT (Ongezeko la Thamani – asilimia 18) na import duties (ushuru wa forodha – asilimia 10) zinazotozwa katika viunganaishi vya mtungi wa gesi, burners, regulators,” anasema.

Alisema endapo kodi itaondolewa katika viunganishi hivyo, itapunguza gharama za ununuzi wa viunganishi kwa mtumiaji wa kawaida kwa wastani wa asilimia 30.

“Kwa mfano, mtungi pekee wa kilo sita wa Oryx unauzwa Sh20,000, gesi yenyewe inajazwa kwa Sh19,000 na viunganishi vyake ni Sh10,000 kwa hiyo kodi hizo zikiondolewa kwenye viunganishi zitapunguza Sh3,000, sawa na asilimia 30,” alisema Mohammed.

Alisema endapo Serikali itatekeleza ombi hilo la kuondoa kodi, itapunguza gharama ya bidhaa ya LPG hivyo kuongeza idadi ya kaya zinazotumia gesi ya kupikia.

Alipendekeza Serikali kuunda mamlaka itakayosimamia mabadiliko kutoka nishati asilia kwenda nishati mbadala akisema kila sekta kwa sasa inafanya kazi pekee bila chombo kinachoziunganisha, chenye mkakati na malengo ya kufanikisha.

Alizungumzia pia changamoto ya gharama za gesi ikilinganishwa na mkaa na kusema kuna majaribio yanayoendelea ya kiteknolojia kuwezesha matumizi ya gesi majumbani kulipiwa kielektroniki.

“Gesi itumike kama tunavyotumia umeme wa luku, unakuwa na mita unalipa kulingana na uwezo wako, hii ndiyo ‘future’ kwa sababu inaonekana gesi labda ni gharama katika ununuzi wa awali, changamoto ni kodi ya viunganishi na mita hizo, endapo litaangaliwa hili itasaidia,” alisema.

Pendekezo jingine kutoka kwake ni kwa Serikali kuanzisha kanuni zitakazosaidia kusimamia biashara ya mkaa ili kudhibiti kasi ya matumizi hayo chini ya mamlaka aliyopendekeza ianzishwe kwa ajili ya kuratibu biashara hiyo.

Akichangia mada hiyo, Oscar Michael kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), alisema anaamini ipo siku mkaa utaondoka katika matumizi ya kupikia kutokana na kasi ya mapinduzi yanayoendelea kujitokeza kwa sasa katika ugunduzi na ubunifu wa nishati mbadala.

“Mazingira ni suala la kila mtu, siyo mtu mmoja, kila Mtanzania anahusika. Jambo la kutia matumaini ni haya mapinduzi ya ubunifu na ugunduzi unaojitokeza kila siku. Miaka ya nyuma tulitumia kuni kwa sehemu kubwa ya wananchi lakini taratibu tumeanza kuona mapinduzi ya nishati ya gesi, kwa hiyo ukiangalia tangu primitive (kipindi cha ujima) hadi kwa sasa tunaona gesi na miaka ijayo, naamini hatutakuwa na mkaa tena,” alisema.

Advertisement