Kinachofanya Waziri Mkuu Ethiopia awindwe kama adui

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed

Jumuiya ya kimataifa inampongeza, majirani wanamsifu kwa kurudisha uhusiano uliovurugika na kuishi kwa kuwindana kwa muda mrefu, lakini ndani ya Ethiopia kazi kubwa inayofanywa na Waziri Mkuu, Abiy Ahmed inatazamwa tofauti na baadhi ya watu hasa wapinzani wake kisiasa.

Amenusurika katika matukio kadhaa ya kumpindua na mauaji tangu alipochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Aprili, 2018.

Moja ya majaribio ya kumuua ni lile la Juni 23, mwaka jana alipokuwa akihutubia mkutano uliofurika watu ambapo bomu lilirushwa lakini walinzi wake walifanikiwa kumuondoa eneo hilo akiwa salama ingawa watu wawili walipoteza maisha na wengine 100 kujeruhiwa.

Watu watano walitiwa mbaroni na kuhusishwa na jaribio mauaji. Waliohusishwa na tukio hilo walitajwa ni Getu Girma, Birhanu Jafar, Tilahun Getachew, Bahiru Tollosa na Desalegn Teafaye.

Inadaiwa walipohojiwa watu hao walisema kilichowasukuma kufanya hivyo ni hofu yao kwa Abiy kwamba huenda hataweza kulinda maslahi ya kabila kubwa zaidi nchini humo la Oromo katika utawala wake.

Oromo ndilo kabila la Abiy na ndilo lililoendesha shinikizo kwa miaka mitatu mpaka likamng’oa mtangulizi wake, Hailemariam Desalegn aliyejiuzulu mwanzoni mwa mwaka jana.

Waliotiwa mbaroni walidaiwa kushinikiza nchi kuongozwa na mmoja wa watu kutoka kikundi cha wapiganaji wa Oromo cha OLF.

Kwa nini anawindwa?

Moja ya changamoto zinazoikabili Ethiopia ni kuwapo kwa mivutano na wakati mwingine mapigano ya kikabila ambapo Mei mwaka huu kulishuhudiwa mauaji ya watu kadhaa na wengine kujeruhiwa.

Katika vurugu hizo zilizohusisha kikundi cha Amhara na kikundi cha kikabila cha Gumuz, vurugu zilishuhudiwa zikiyakumba majimbo ya Amhara na jimbo jirani la Benishangul Gumuz.

Mbali na vurugu za kikabila, inadaiwa ndani ya jeshi la Ethiopia bado kuna kundi kubwa la wanajeshi lenye mtazamo tofauti dhidi ya Waziri Mkuu Abiy.

Oktoba mwaka jana Aby alisema kikundi cha wanajeshi kilifika ofisini kwake kwa madai ya kutaka kuwasilisha kilio cha kuongezewa mshahara, kilikuwa na lengo la kumuua.

Aidha, Abiy amejitengenezea maadui baada ya kuwa na msimamo wa kukomesha rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ambao awali ulikuwa ukilalamikiwa kwa wingi nchini humo, hivyo kuwa kikwazo kwa baadhi ya watu waliozoea na kuuona ni sehemu ya maisha yao.

Takribani maofisa 60 wakiwamo wanajeshi na wana intelejensia walikamatwa mwaka jana miongoni mwao akiwamo naibu kiongozi wa usalama wa zamani na kiongozi mwenye wadhifa wa juu katika jeshi.

Aidha, jimbo la Amhara limekuwa likitazamwa kwa karibu na kwa umuhimu nchini Ethiopia kutoakana na kuwa makao ya kundi kubwa la kikabila la Amhara ambalo limetoa lugha ya Taifa ya Amharic.

Aliyepanga mapinduzi

Ofisi ya Abiy imemtuhumu mkuu wa usalama wa jimbo la Amhara, Brigedia Jenerali Asaminew Tsige, kuhusika na mipango ya mapinduzi hayo yaliyoshindwa ambaye awali taarifa zilisema hajulikani alipo lakini baadae ikaelezwa naye ameuawa.

Brigedia Jenerali Asaminew alikuwa mmoja wa maofisa wa juu wa jeshi waliochiliwa kutoka gerezani mwanzoni mwa mwaka jana baada ya kukaa huko kwa karibu mwongo mzima akituhumiwa kutaka kupindua Serikali.

Hata hivyo, Serikali ilimwachia yeye na wenzake ili kufungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini humo na kuongeza kasi ya demokrasia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, waliotekeleza mkakati wa kupindua Serikali ya jimbo la Amhara walimuua Gavana wa jimbo hilo pamoja na maofisa wengine waliokuwa kwenye kikao.

Dalili za kutokea tukio kama hilo katika jimbo la Amhara zilionekana mapema baada ya mwanzoni mwa mwezi huu brigedia jenerali huyo kurekodi video na kuisambaza kupitia mtandao wa Facebook akiwataka wananchi kujiandaa.

Jinsi mkuu wa majeshi alivyouawa

Jenerali Seare Mekonnen aliuawa na mlinzi wake Jumamosi jioni saa kadhaa baada ya tukio la mapinduzi yaliyoshindwa huko Amhara.

Mauaji yake yananasibishwa na mpango wa mapinduzi ambapo wauaji walimtumia mlinzi huyo kumpiga risasi Seare aliyekuwa akizungumza na mgeni aliyemtembelea, brigedia Gezai Abera.

Serikali inasema kuna kila sababu ya kuyahusisha mauaji ya Seare na Gavana wa Amhara katika shambulio ambalo lilimjeruhi mwanasheria mkuu wa jimbo hilo ambaye baadae alifariki dunia, pia wauaji walimuua mshauri mwandamizi wa gavana huyo Ezez Wasie.

Sehemu kubwa ya walioshiriki katika mpango huo wa mapinduzi wametiwa mbaroni na wanashikiliwa na vyombo husika wakati uchunguzi zaidi ukifanyika kabla ya kuendelea na hatua zingine za kisheria dhidi yao.

“Mapinduzi ya kijeshi waliyotaka kuyatekeleza Amhara ni kinyume cha katiba na yamelenga kudidimiza hatua kubwa ya mafanikio kiusalama yaliyofikiwa.

“Jaribio hili la mapinduzi lazima lilaaniwe na Waethiopia wote, Serikali kuu inao uwezo wa kutosha kukabiliana na vikundi vyenye silaha,” ilisema sehemu ya taarifa ya Serikali.

Seare alidumu katika nafasi ya mkuu wa majeshi kwa mwaka mmoja tu tangu alipoteuliwa na Abiy alipokalia kiti hicho ambacho ndicho cha juu kwa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za kiserikali katika Taifa hilo.

Inaelezwa kwamba wauaji walimuua Gavana wa Amhara na mkuu huyo wa majeshi kwa kuwa ni nguzo muhimu kwa Abiy aliyefanikiwa kurudisha uhusiano na Eritrea ambao ulitetereka kwa muda mrefu na kuzifanya nchi hizo jirani kukatisha uhusiano wa kidiplomasia.

Mbali na Eritrea, hivi karibuni Aby ambaye pia ni Mwenyekiti wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo kwa Pembe ya Afrika (Igad), alijitosa kuwa msuluhisi wa mgogoro wa Sudan ambao umeendelea kupitia hatua mbalimbali hata baada ya kungg’olewa kwa kiongozi wake wa muda mrefu, Omar al-Bashir aliyekuyekuwa akilalamikiwa kukandamiza demokrasia nchini mwake.