Kirusi cha HPV hatari kwa wanawake

Muktasari:

  • Mwathirika wa HPV hupunguza kinga ya kupigana na maradhi mengine

Maradhi ya zinaa ya Human Papilloma Virus (HPV) ni miongoni mwa magonjwa yanayosambazwa kwa njia ya kujamiiana.

Wanawake wengi wenye maradhi hayo wapo katika hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Mtaalamu wa magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, Dk Nestory Masalu anasema kirusi hicho bado hakina tiba na kinasambazwa kupitia sehemu za siri.

Bila kutaja idadi ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo wakiwa na maradhi ya HPV kwa siku au baada ya muda fulani, anasema maradhi hayo yamekuwa tishio miongoni mwa watu hasa walio katika uhusiano wa kimapenzi.

Anasema karibia asilimia 50 ya wahusika wa tendo la ndoa hupata matatizo hayo.

“Janga la VVU (Virusi vya Ukimwi), limekuwa gumzo kiasi kwamba tunasahau baadhi ya maradhi mengine ambayo ni hatari sana. HPV pia ni tishio kwa sasa maana hamna tiba ambayo imepatikana,” anasema Dk Masalu.

Anafafanua kuwa kutokana na kirusi hicho, saratani ya mlango wa kizazi imekuwa sugu miongoni mwa wanawake nchini ambayo imesababisha karibia kesi zote za maradhi.

Aliyekuwa mganga mfawidhi wa Hospitali ya Nyamgana, Agnes Mwita, ametaja baadhi ya dalili za HPV kuwa ni pamoja na vinundu vidogo kwenye ngozi sehemu za siri na wakati mwingine sehemu zingine za mwili.

Anasema mwathirika wa HPV yupo katika nafasi kubwa ya kupata maradhi mengine ya zinaa hasa VVU.

“Tofauti na maradhi mengine ya zinaa, HPV inasababisha matatizo makubwa na kibaya zaidi huwa haitambuliki kwa haraka. Wanaume pia hupata maradhi haya ingawa kwa Tanzania bado kesi ni chache,” anasema Dk Mwita.

“Licha ya tatizo hili la HPV kuwa kubwa, watanzani wengi hawana uelewa wowote kuuhusu na namna ya kujikinga.”

Dk Mwita anasema mara nyingi ugonjwa huu unasababishwa na kusambazwa na ngono zembe miongoni mwa vijana.

“Mwathirika wa HPV hupunguza kinga ya kupigana na maradhi mengine na hivyo kudhoofu kiafya,” anasema Dk Mwita.

Baadhi ya wakazi wa Mwanza wanasema Serikali ilapaswa kutoa elimu ya kutosha hasa kwa watu waishio vijijini ili wawe katika ufahamu wa athari za maradhi hatari kama vile saratani.

“Serikali ilipaswa kujenga vituo vingi vya kupima maradhi hatari kama vile saratani na kutoa elimu ya umuhimu wa kupima kwa hiari kwa lengo la kuzuia vifo visivyokuwa vya lazima,” anasema Zuwena Faridi, mkazi wa Mwanza.