Lwakatare ajitenga na uvumi kuhamia CUF

Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare

Muktasari:

  • Uvumi kuwa Wilfred Lwakatare Mbunge wa Bukoba Mjini kutimkia Cuf umeanza kusambaa leo Jumapili asubuhi huku akidai alisalimiana na Mwenyekiti wa Cuf ofisini kwake Profesa Ibrahimu Lipumba alipokuwa akitokea kwa rafiki yake mwenye makazi karibu na ofisi hizo.

Bukoba. Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare kupitia Chadema amejitenga na uvumi unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa amejiunga na Chama cha Wananchi (CUF) akidai bado anawaheshimu wapiga kura wake.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Juni 9,2019, amesema ni kweli jana alifika kwenye ofisi za CUF pale Buguruni Dar es Salaam akitoka kwenye tukio la kifamilia la mwanasiasa rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Shoka.

Kwamba, makazi ya rafiki yake yapo karibu na zilipo ofisi za CUF, wakati anaondoka kabla ya kupanda gari walimiminika wanachama na viongozi wa chama hicho wakimtaja kama Naibu Katibu Mkuu wao wa zamani.

Amedai wananchi hao walikuwa wanaondoka baada ya kumaliza kongamano lao lakini walimuomba aingie ofisini na kusalimiana na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba.

“Gari langu niliegesha karibu na ofisi za CUF nilipofika, wakati naondoka walikuwa wamemaliza kongamano lao wakaomba nikamsalimie Profesa Lipumba, nikaingia ndani ya 'gate' sikuona tatizo,” amefafanua Lwakatare.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo alitumia dakika 10. Anasema aliondoka CUF kwa misingi na sasa yupo kwenye chama kingine alichosema anakitumikia kwa uaminifu na kuwaheshimu wapiga kura wake.

Aidha, Lwakatare amedai si mara ya kwanza kuzushiwa kukihama chama chake na hivi karibuni alihusishwa na kujiunga na CCM.

Hata hivyo anasema binafsi anaamini katika suala la kupunguza maadui na kuongeza marafiki.

Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Bukoba, Victor Sherejei alisema uvumi huo umeleta taharuki kwa wananchi wa Bukoba na kuwa, mbunge huyo alikuwa anasubiriwa kutoa ufafanuzi wa madai hayo.