Mama atelekeza mtoto stendi Dar, apelekwa kituo cha kulelea yatima

Mkazi wa jiji la Dar es Salaam, Zaituni Omary akimywesha maziwa mtoto aliyetelekezwa katika kituo cha Mabasi cha Ubungo jijini Dar es Salaam jana, kushoto ni Mkuu wa Kituo cha polisi Ubungo, Sara Bundala. Picha na Tumaini Msowoya

Dar es Salaam. Mtoto aliyetelekezwa na mama yake katika kituo cha mabasi cha Ubungo amekabidhiwa katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Maria Theresa kilichopo Mburahati, jijini Dar es Salaam.

Mtoto huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miezi mitatu hadi minne, alitelekezwa jana baada ya mama yake aliyekuwa kwenye banda la kupumzikia abiria kumuomba jirani yake amshikie kwa madai anakwenda kujisaidia, lakini hakurudi.

Akisimulia tukio hilo, abiria aliyekabidhiwa mtoto huyo, Mary Gasper alisema alifajiri ya jana akiwa kwenye banda la kupumzikia wageni, mama mmoja alimuomba amshikie mwanaye.

“Aliponipatia mtoto alinipa pia mkoba wenye nguo akisema atarudi, nilimsubiri kwa zaidi ya saa moja bila mafanikio ikabidi niende kutoa taarifa kwenye jengo la utawala ili watangaze,” alisema Mary.

Abiria huyo alisema alilala kwenye kituo hicho cha mabasi baada ya kuwasili usiku wa manane na basi la ABS akitokea Tabora.

“Nilikuja usiku nikitokea Tabora, sikuweza kurudi nyumbani hivyo nililala hapahapa nikisubiri kukuche ndio huyu mama alikuja na kunipatia mtoto,” alisema Mary.

Meneja wa kituo hicho, Imani Ernest baada ya kutangaza kupitia spika zilizo kwenye kituo hicho bila mafanikio alitoa taarifa polisi akiomba msaada zaidi.

Alisema wakati matangazo hayo yakiendelea walimpatia mtoto huyo maziwa na kumbadilisha nguo kwa sababu alikuwa akilia kwa njaa.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Ubungo, Michael Ayoub alisema tayari mtoto huyo ameshapokewa kwenye kituo cha kulelea watoto yatima na kwa sasa wanasubiri ndugu au mama yake ajitokeze.

Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Palestina, Delila Moshi alisema mtoto huyo hana matatizo yoyote kiafya.

“Ana mafua ambayo yatapona, afya yake ni nzuri na anaweza kuendelea kulelewa kwenye kituo bila wasiwasi wowote ule,” alisisitiza daktari huyo ambaye kabla ya kumpima mtoto alimsafisha na kumpatia maziwa huku akimbembeleza kwa sababu muda mwingi alikuwa akilia.

Mkuu wa kituo cha Polisi Ubungo, Sara Bundala alisema wanaendelea kumtafuta mama wa mtoto huyo.

“Nilipopewa hizi taarifa niliwatafuta maofisa ustawi wa jamii nikawakabidhi mtoto, anaendelea vizuri kwa sasa,” alisema.

John Paul, mchungaji wa kanisa la Jehova Mercy ambaye hutoa huduma ya maombi kwenye kituo hicho alisema zipo sababu nyingi zinazowafanya wanawake hasa walio kwenye umri mdogo kutelekeza watoto.

Alisema moja ya sababu hizo ni kukataliwa na wenza wao baada ya kupata ujauzito huku wakikabiliwa na ugumu wa maisha bila kuwa na suluhisho.