Mwalimu mstaafu atapeliwa Sh60 milioni za mafao

Muktasari:

  • Polisi mkoani Morogoro linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kumtapeli mwalimu mstaafu mkazi wa Kiberege wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro Sh60 milioni ambazo ni mafao yake ya uzeeni.

Morogoro. Mwalimu mstaafu mkazi wa Kiberege wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ametapeliwa pesa taslimu Sh60 milioni ambazo ni fedha za mafao na watu watatu waliojitambulisha kwake ni wafanyabiashara wa madini ya dhahabu.

Watu hao walidai kuwa soko lao lipo kwa mapadri wa kanisa la Mtakatifu Patrick mjini Morogoro.

 Matapeli hao walikutana na mstaafu huyo Julai 20 mwaka 2019  maeneo ya Benki ya NMB tawi la Ifakara na kumtaka wafanye biashara ya madini ya dhahabu na baadaye waliondoka naye hadi mjini Morogoro kwa ajili ya kufanya makubaliano ya biashara hiyo.

Akizungumzia tukio hilo jana Ijumaa Julai 26,2019, kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa aliwataja watuhumiwa hao ni Shabii Rajabu, Mnyakile Luoga na Maulid Msiku aliyejitambulisha ni mhasibu wa kanisa la St. Patric jambo ambalo sio kweli.

Kamanda huyo  alisema baada ya kufika mjini Morogoro mstaafu huyo alikwenda na matapeli hao benki ya NMB na kutoa pesa katika akaunti yake kiasi cha Sh60 milioni na kuwakabidhi matapeli hao na kumpatia madini ya dhahabu feki yakiwa kwenye maboksi madogo matatu yaliyokuwa yamezungushiwa utepe mweusi.

Alisema baada ya kupata kiasi hicho cha fedha matapeli hao waliokuwa na gari ndogo aina ya Noah walimshusha mstaafu huyo kwenye gari na kutoweka kusikojulikana.

Kamanda Mutafungwa alisema baada ya mstaafu huyo kufungua maboksi hayo alikutana na gololi za baiskeli na sio madini ya dhahabu hivyo alitoa taarifa kituo cha polisi Morogoro kuwa ametapeliwa na upelelezi ulianza na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja anayeitwa Shabii Rajabu mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa katika nyumba ya kulala wageni maeneo ya nanenane mjini Morogoro na alipofanyiwa upekuzi alikutwa akiwa na kiasi cha pesa taslimu Sh11.3 milioni kati ya Sh60 milioni alizotapeliwa mstaafu.

Aidha alisema mstaafu huyo aliweza kumtambua mtuhumiwa huyo kuwa ni miongoni mwa matapeli waliomuibia fedha hizo ambazo ni mafao yake ya kustaafu.

Baada ya kukamatwa mtuhumiwa alihojiwa na alikiri kwamba alihusika katika tukio hilo la utapeli na alipata mgao wa Sh. 15 milioni.

Kamanda Mutafungwa alisema wanaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine pamoja na pesa zilizobaki za kumpeleka mahakamani zinafuata mara baada ya upelelezi utakapokamilika.

Kufuatia tukio hilo, Kamanda Mutafungwa aliwataka wananchi hasa wastaafu kuacha tamaa za kununua madini kiholela kwa dhana ya kupata fedha badala yake waende ofisi za madini kwa usalama na uhakika wa fedha zao.