VIDEO: Alichokisema Zitto mbele ya Maalim Seif

Muktasari:

  • Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia katika chama hicho ni mwendelezo wa kudai haki ya wananchi wanyonge na si kuvunja sheria za nchi

Unguja. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia katika chama hicho ni mwendelezo wa kudai haki ya wananchi wanyonge, si kuvunja sheria za nchi.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini ametoa kauli hiyo leo katika ofisi mpya za ACT zilizopo Vuga, Unguja ambazo awali zilikuwa makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar.

Leo kwa mara ya kwanza tangu alipohamia ACT, Maalim Seif ambaye alikuwa katibu mkuu wa CUF amefika katika ofisi hizo na kulakiwa na viongozi mbalimbali ambao pia wamehama CUF na kujiunga na chama hicho.

Zitto amesema kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa nchini, ACT kinafuata kanuni, sheria na taratibu bila kubughudhi mtu.

Amesema lengo la chama hicho si kuanza malumbano yasiyo ya msingi na Serikali, bali ni kuanza mapambano ya kujizolea wanachama wapya.

Katika kufanikisha hilo, kiongozi huyo wa ACT amesema watafanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba kwa siku nne.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kuzungumza na wanachama wapya sambamba na kutoa kadi.

"Niwaombe wananchi msichokozwe mkachokozeka au kwenda kinyume na sheria. Malengo yetu ya kusonga mbele kisiasa yaweze kutimia,” amesema Zitto.