Vimbunga viwili vyazuia mvua nchini

Muktasari:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yaeleza kilivyoathiri mifumo inayosababisha mvua

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetaja sababu za uhaba wa mvua katika baadhi ya maeneo nchini kuwa unatokana na vimbunga viwili vilivyozishambulia nchi jirani za Kusini.

Nchi hizo ni Msumbiji, Zambia na Malawi ambako pia watu wengi wamepoteza maisha na wengine kukosa makazi kutokana kimbunga kinachoitwa Idai.

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa TMA, Samwel Mbuya aliliambia Mwananchi jana kuwa mgandamizo mdogo wa hewa uliojitokeza Mashariki mwa Madagascar pamoja na kimbunga cha Savana na Idai vimeathiri mifumo ya hali ya hewa na unyeshaji wa mvua za msimu nchini.

Alisema mikoa ambayo imeathirika kwa kiwango kikubwa ni ya Morogoro (upande wa Kaskazini), Pwani, Tanga, Manyara na Kilimanjaro.

Alisema kimbunga Savana ambacho kitakufa kabla hakijafika Mashariki ya Madagascar pamoja na kimbunga Idai kilichotokea nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe vimeathiri mfumo wa mvua katika kipindi cha hivi karibuni.

Mbuya alisema mikoa hiyo itakuwa na upungufu wa mvua kwa kipindi hiki, hivyo wakulima wanashauriwa kulima mazao ya muda mfupi.

Alisema katika Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa Victoria, mvua za msimu zinaendelea kunyesha kama ilivyotarajiwa.

Meneja huyo alisema kimbunga Idai kilisababishwa na mgandamizo wa hewa uliojitokeza katika ukanda wa Madagascar kilianza Machi 5 hadi 15, lakini kimesababisha mafuriko katika nchi hizo tatu.

“Kwa upande wa Tanzania hakuna tatizo lolote la kutokea kwa kimbunga hicho katika maeneo yetu, hivyo kuna kimbunga cha Savana ambacho kitakufa mapema kabla ya kufika Mashariki mwa Madagascar,” alisema Mbuya.

Kimbunga Idai kilipiga Pwani ya Beira, Msumbiji Alhamisi wiki iliyopita kikiwa na upepo uliovuma kwa kasi ya kilomita 200 kwa saa kabla ya kuelekea Magharibi katika nchi za Malawi na Zambia.

Serikali ya Msumbiji imesema watu 84 wamethibitika kufariki dunia na wengine 100,000 waliokolewa kwa dharura.

Huko Zimbabwe zaidi ya watu 100 wamethibitika kupoteza maisha kwa mujibu wa mamlaka za Serikali ya nchi hiyo.

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Msumbiji lilisema takriban watu 400,000 hawana makazi kufuatia athari za kimbunga Idai.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Tanzania ilitoa msaada wa chakula na dawa kwa nchi hizo ambacho Serikali iliwakabidhi mabalozi wa nchi hizo katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.