Wananchi wasota saa 15 kukatika daraja Tambani, Waziri Ulega aahidi daraja la muda 

Muktasari:

  • Wananchi wanavushwa kwa kati ya Sh300 hadi Sh500 kwa mtu mmoja na vijana walioweka mbao na ngazi kwenye eneo hilo.

Temeke. Mamia ya wananchi wamesota kwa takribani saa 15 kutokana na daraja la Kifaulongo katika Kata ya Tambani mkoani Pwani kukatika na kusababisha adha kwa watumiaji wa eneo hilo.

Daraja hilo limekatika saa moja usiku jana Ijumaa Aprili 26, 2024 kutokana mvua zilizokuwa zimenyesha maeneo mbalimbali ikiwemo mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Mwananchi Digital lililokuwa limeweka kambi eneo hilo tangu asubuhi ya leo Jumamosi, Aprili 27, 2024 limeshuhudia kina mama wenye watoto wakihangaika kutaka kuvuka kwenye maji ili kwenda upande wa Mbande, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kupata huduma za afya.

Wananchi wamelazimika kuweka magogo, ngazi na kuvushana kwa wanaoweza, huku  wengine walinusurika kusombwa na maji. Hata hivyo baadaye  walioruhusiwa kupita ni wenye dharura za msingi ili kuepusha maafa.

Mkazi wa Tambani Shule, Adelina Kisaka amesema amefika hapo tangu saa 12  asubuhi akitaka kwenda kumpeleka mtoto wake hospitali, hata hivyo amekwama kutokana na kukatika daraja hilo.

Amesema kulikuwa na vijana waliojitolea kwa kuweka daraja lakini hata hivyo ameshindwa kuvuka kutokana na kuogopa kwani ni hatari kwa usalama wake na mtoto.

"Nimekuta vijana wamejitolea wanavusha watu kwa Sh1,000 hata hivyo, nimeshindwa kwa sababu hata eneo lenyewe walilolaza ngazi linakaribia kuanguka," amesema Kisaka.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Khamis Kato amesema ndugu zao na jamaa wameshindwa kushiriki msiba ambao upo nyumbani kwao Kijiji cha Mkoga.

"Huu msiba umetokea tangu jana hata hivyo gari lililobeba waombolezaji kutoka Kigamboni imekwama hapa darajani na hivyo tunaangalia namna nyingine ya kuzunguka ili waweze kuwahi mazishi."

Adha hiyo imemfikisha eneo hilo,  Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Mkuranga kujionea hali ilivyo.

Ulega amefika na msafara wa magari manne katika eneo hilo saa 4:50 asubuhi na kuwapa pole wananchi waliokwama katika daraja hilo.

Akizungumza na wananchi waliokuwa upande Temeke kisha kuvuka kwa kutumia ngazi huku akishuka kwa tabu ili kwenda upande wa Tambani, amesema Serikali imechukua hatua za dharura ikiwamo  kuagiza lijengwe daraja la muda kwa kujaza mawe eneo lililokatika kisha kuwekwa daraja la mbao.

"Ninawapa pole wananchi waliokumbwa na kadhia na hadi kufikia saa 10 jioni leo Jumamosi ninaamini mawasiliano yatarejea," amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga, Amani Kamwaga amesema wamepokea maagizo ya mbunge na utekelezaji umeanza.

Amesema mbunge amechangia Sh300,000 kwa ajili ya kununua mbao za kutengenezea daraja la muda.

"Muda huu kuna vijana wamejitolea kuvusha wananchi kwa gharama ya Sh200 hadi Sh500 lakini mpaka jioni tukikamilisha hawataendelea kuwatoza wananchi nauli ya kuvukia.