Tambani waomba kujengewa daraja Bonde la Mkoga

Pwani. Wakazi wa Kata ya Tambani Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wameiomba Serikali kuwatengenezea daraja katika Bonde la Mkoga ili kuepuka adha ya kuvuka kwa kutumia maboya na mitumbwi pindi maji yanapojaa kwenye mto huo.

Wakazi hao wamedai kuwa wanakutana na changamoto kubwa hasa kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwananchi ilifika katika bonde hilo na kushuhudia watu wakivushwa kwenda upande wa pili kwa kutumia maboya ya plastiki na vivuko vilivyotengenezwa kwa mbao na madumu ya maji.

Miongoni mwa waliokuwa wakivuka ni wanafunzi ambao wanasoma upande wa pili wa bonde hilo katika Shule ya Msingi Mbande ambayo ipo jirani na Kata ya Tambani.

Mmoja wa wakazi hao, Andrew Kajuna alisema wamekuwa wakipitia changamoto hiyo kwa muda mrefu na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kukabilina na hali hiyo.

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya Saku, Gervas William ambaye amesema wapo wanafunzi wanaoshindwa kwenda shule kwa kuhofia kuvuka bonde hilo kwa maboya.

Mwananchi lilizungumza na William Mwamboneko ambaye ni mmiliki wa maboya yanayotumika kuvusha watu.

Alisema ameweka maboya kuvusha watu ili kusaidia changamoto ya watu kupita kwenye maji wakati wa kwenda na kurudi kutoka kwenye shughuli zao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde alisema halmashauri yake inafahamu kuhusu tatizo hilo na inaendelea kulipatia ufumbuzi.

“Hili suala si la wilaya moja, hilo bonde tunapakana na wenzetu wa Ilala hivyo kwa upande wetu nimeshazungumza na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) Mkuranga ili wakutane na Tarura wa Dar wajadili kuona ni namna gani wanaweza kuboresha miundombinu ya eneo hilo,” alisema.