Wizi wa njia ya simu watikisa Kilimanjaro

Moshi. Wizi kwa njia ya mitandao ya simu unazidi kutikisa mkoa wa Kilimanjaro, huku mawakala wanaotoa huduma ya kutoa fedha wakitajwa kuchangia kushamiri kwa wizi huo kwa kutoa fedha kiholela.

Kutokana na hali hiyo, jeshi la polisi limewatangazia kiama mawakala ambao watabainika fedha zilizoibwa kwa njia ya mtandao zilitolewa katika maeneo yao.

Utaratibu unataka wakala aandike kumbukumbu za mtu anayetoa fedha ikiwamo namba yake ya simu, namba ya kitambulisho chake, kiasi alichotoa na muda aliotoa fedha na kuweka sahihi yake.

Akizungumza mjini hapa mwishoni mwa wiki, kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita aliwaonya mawakala wanaotoa fedha bila kufuata utaratibu kuwa nao sasa wataunganishwa katika kesi za wizi wa kimtandao.

“Baadhi yao wamekuwa sehemu ya mtandao huu wa wizi. Tukikukuta umetoa fedha iliyoibwa kwa njia ya mtandao na huna kumbukumbu za mtoaji basi na wewe ni sehemu ya uhalifu. Tutakubeba.”

“Jana tu (juzi) kuna mtu amepigwa Sh 700,000 kwa njia ya mtandao. Tumefuatilia tumempata wakala tunamuuliza uliandika wapi kumbukumbu, alikupa kitambulisho gani vyote hakufanya.”

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini mawakala wengi kama si wote walioko mitaani na kwenye miavuli, hawafuati utaratibu huo na wamekuwa wakitoa hadi Sh1 milioni bila kuhoji kitambulisho.

“Utaratibu uko wazi kwamba wanatakiwa waingize data za anayetoa fedha na mtoaji aweke sahihi yake lakini wanatoa fedha kienyeji. Hawa ndio kiini cha kushamiri wizi huu,” alisema ofisa mmoja wa polisi.

Mmoja wa mawakala wakubwa wa miamala ya fedha kwa njia ya mtandao mkoani Kilimanjaro, Patrick Boisafi alikiri mawakala wengi wadogo mitaani wanakiuka taratibu katika utoaji wa fedha.

Mfanyabiashara, Patrick Kennedy anayemiliki duka stendi kuu ya mabasi Moshi ambaye pia ni wakala naye alikiri mawakala wengi kutofuata taratibu zinazotaka watunze kumbukumbu.