Mtoto aliyekatwa koromeo wilayani Njombe afariki dunia

Muktasari:

Meshack Myonga (4),  aliyenusurika  kuuawa baada ya kutekwa na kukatwa koromeo wilayani Njombe amefariki dunia leo mchana Jumamosi Februari 9, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya

Njombe.  Meshack Myonga (4),  aliyenusurika  kuuawa baada ya kutekwa na kukatwa koromeo wilayani Njombe amefariki dunia leo mchana Jumamosi Februari 9, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Desemba 23, 2018  mtoto huyo alitekwa na mtu asiyejulikana  akiwa  nyumbani kwa wazazi wake mtaa wa Mji Mwema wilayani Njombe, kisha kupelekwa msituni na kukatwa  koromeo kabla ya kuokolewa na kijana mmoja.
Baada ya kuokolewa alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Kibena-Njombe na baadaye  kuhamishiwa hospitali ya rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.

Akizungumza na Mwananchi mama mzazi wa mtoto huyo, Rabia Mlelwa amesema, "Leo tumekwenda Hospitali na madaktari wakamchukua wakaingia chumba cha matibabu, baadae nikaitwa na kuambiwa mtoto amefariki. Hata sielewi imekuaje."

"Wakati wanaingia nae ndani  hawakuniambia lolote kuhusu maendeleo yake ila waliniambia mwanangu amefariki, wamesema mtoto koromeo lake lilikuwa limekaa vibaya hivyo alikuwa mtu wa kufa muda wowote."

Amesema alipewa taarifa za kifo cha mwanaye saa nane mchana, kuelezwa koromeo  lilikuwa limesinyaa.

Amebainisha kuwa jana ndio alitakiwa  kurudi katika hospitali hiyo kujua maendeleo ya mwanaye   baada ya kukaa wiki mbili katika hospitali hiyo ya rufaa wakipatiwa matibabu.

"Jana Mkuu wa wilaya ya Njombe (Ruth Msafiri) alitoa gari lililotuleta Mbeya, lakini leo baada ya tukio hili ametaarifiwa hivyo ameamuru gari hilo lirudi tena kwa ajili ya kutuchukua hivyo kesho asubuhi ndiyo tutaanza safari kurudi kijijini Ngalangwa (Njombe)," amesema.