Kesi ya ‘house ‘boy’ kudaiwa kumuua ‘house girl’ yanguruma

Muktasari:

  • Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Jumatatu iliyopita na Jaji Yose Mlyambina katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kimya cha takriban miaka sita.

Dar es Salaam. Shahidi wa pili katika kesi ya mauaji ya mfanyakazi wa ndani wa kike wa Jaji mstaafu, Engela Kileo anayedaiwa kuuawa na mfanyakazi mwenzake wa ndani wa kiume, ameileza Mahakama kilichowasukuma kufanya upekuzi chumbani kwa mshtakiwa na kukuta mabegi ya nguo za marehemu na simu.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 96 ya mwaka 2016, mshtakiwa Philemon Laizer anadaiwa kumuua Lucy Maina kwa kukusudia. Philemon mwenyeji wa Arusha na Lucy ambaye alikuwa raia wa Kenya walikuwa wafanyakazi nyumbani kwa Jaji Kileo.

Philemon anadaiwa kumuua Lucy Juni 8, 2013 usiku wa manane nje kidogo ya nyumba hiyo waliyokuwa wakifanya kazi Mikocheni B jijini Dar es Salaam kutokana na sababu za kimapenzi na kisha kuutupa mwili kichakani.

Shahidi huyo ambaye kwa sasa ni mkuu wa upelelezi mkoa wa Kigoma (RCO), mrakibu mwandamizi wa polisi, Mark Njela aliieleza:“Tulipotaka kwenda chumbani kwake kwanza alikataa Jaji (Kileo) ndio akamwambia wape nafasi. Tulipoingia tulikuta vitu mbalimbali. Kulikuwa na mabegi mawili ya nguo na mfuko wa nailoni yakiwa na nguo, viatu na simu ya SamSung vikiwa uvunguni mwa kitanda.”

“Tulipomuuliza mtuhumiwa vitu hivyo vilifikaje chumbani mwake baada ya kuvuta pumzi ndefu sana akakiri kwamba ni amehusika na mauaji hayo.”

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Jumatatu iliyopita na Jaji Yose Mlyambina katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kimya cha takriban miaka sita.