Spika mstaafu Anna Makinda atoa neno nafasi za ubunge 2020 kwa wanawake

Muktasari:

Spika mstaafu Anna Makinda anatamani kuona idadi ya wabunge wanawake wanaotokana na majimbo wanaongezeka


Dar es Salaam.  Spika mstaafu wa Bunge Anna Makinda amewataka wabunge wanawake kuhakikisha kwenye Bunge lijalo idadi ya wabunge wanawake ndani wanaongezeka.

Makinda aliyasema hayo jana Alhamisi Machi 7, 2019 jijini Dar es Salaam alipozungumza na wadau wa masuala ya wanawake katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) na Oxfam.

Mkutano huo ulijadili namna ya kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa  mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2020.

Alisema Bunge la sasa lina wabunge wanawake wa majimbo asilimia 6.7 pekee, kiasi ambach kiko chini sana.

Alisema kama isingekuwa ni matakwa ya sheria kuruhusu wabunge wa viti maalumu, wanawake wangekuwa wachache bungeni.

 

“Wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi na wajiandikishe kupiga kura. Wasivamie tu siasa, siasa ni hesabu, hujafanya hesabu siasa huwezi,” alisema Makinda.

 

Alisema haoni sababu ya wanawake kushindwa kama watafanya hesabu vizuri wakitaka kugombea.

 

Makinda alisema wanawake wanatakiwa kujengewa ari ya kujiamini na suala hilo ni endelevu siyo la muda mfupi.

 

Spika huyo mstaafu alisema kamati kuu nyingi za vyama vya siasa zina wajumbe wengi wanaume, jambo linalowafanya wasiwape wanawake nafasi za kugombea nafasi za uongozi kwenye mitaa, kata na majimbo.

Alisema upungufu wa wabunge wanawake majimboni unaanzia kwenye vyama vya siasa ambavyo kamati kuu zake zinapitisha majina ya wanaume wengi kwa kuhofia kupoteza kwenye chaguzi iwapo watasimamisha wanawake.

“Wakati mwingine wanasema tukimweka mwanamke tutapoteza. Lakini wanatakiwa kutambua kwamba wanawake wana uwezo mkubwa wakipewa nafasi na tunashuhudia wanawake walio kwenye nafasi za uongozi wameacha alama kwenye nafasi zao,” amesema Makinda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tawla, Tike Mwambipile alisema wamebaini kwamba ushiriki wa wanawake kwenye vyombo vya uamuzi ni mdogo, hivyo wamejipanga kuwahamasisha ili kuongeza ushiriki wao.

“Wanawake tunakabiliwa na changamoto nyingi hasa linapokuja suala la kushiriki kwenye vyombo vya uamuzi. Wakati mwingine wanawake tuna matatizo yetu lakini mfumo dume ndiyo umekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya jamii,” alisema Mwambipile.

Mbunge wa Hanang Mary Nagu alisema suala la uongozi kwa wanawake liko kwao wenyewe, wanatakiwa wajiamini na wawe na mikakati ya kufikia malengo yao. Amewataka wajue sifa zao na namna ya kuzielezea sifa hizo kwa watu ili wakubalike. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema mamlaka za uteuzi nazo zitambue kwamba wapo wanawake wengi wenye uwezo, hivyo wapewe nafasi ya kufanya kazi.