Mshahara wa Jafo waibua mvutano mkali wabunge wa CCM, Chadema

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffar Michael ameibua hoja ya kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya Bunge zima kupitia kifungu hadi kifungu bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2019/20.

Dodoma. Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffar Michael ameshika shilingi ya mshahara wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo akitaka Serikali iondoe zuio la mikutano ya hadhara wakati nchi inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mbunge huyo ameyasema hayo jana jioni Jumatatu Aprili 15, 2019 Bunge lilipokaa kama kamati ya Bunge zima kupitia kifungu kwa kifungu bajeti ya Ofisi ya Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Michael alisema limetolewa tangazo la Serikali kuwa uchaguzi utafanyika Oktoba 2019.

“Watu waruhusiwe kufanya mikutano ya kisiasa kama vyama vya siasa havifanyi mikutano utakuaje na usawa. Serikali itoe tangazo kuondoa zuio la kufanya mikutano ili watu wajiandae na  uchaguzi,” amesema.

Akijibu hoja hiyo, Jafo amesema mchakato wa uandikishaji na kampeni na kipindi cha kampeni kimeonyeshwa hivyo jambo hilo haliko vibaya.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Aida Kanani ameunga mkono Michael kwamba kufanya uchaguzi si kufanya uteuzi.

Kanani amesema kabla ya kufanya uchaguzi kwa namna yoyote lazima zifanyike shughuli mbalimbali ikiwamo mikutano ya hadhara.

“Kama kweli unaamini kama ushindi upo huwezi kujipigia wewe mwenyewe,  waache vyama vifanye kazi,” amesema.

Mbunge wa Serengeti (CCM), Chacha Marwa amesema kilichozuia ni mikutano kabla ya kampeni na ratiba za kufanya kampeni ziko kwenye utaratibu wake na zimetolewa.

Ryoba amesema ili chama kishinde uchaguzi lazima kiwe na mzizi na kutaka Chadema kujijenga kwa kutumia utaratibu huo kwani hakuna anayezuia.

“Unataka kwenda kufanya kampeni kwa nani? Mikutano isifanyike hadi kampeni zitakapoanza,” amesema Marwa aliyewahi kuwa mbunge wa Chadema kabla ya kujiuzulu na kuhamia CCM.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Lucy Magereri amesema siku saba zilizotolewa  kwa ajili ya kampeni hazijitoshi kujitangaza, kujieleza na kueleweka.

“Sheria ipi inazuia vyama vyenye uwakilishi na ambavyo havina uwakilishi bungeni kufanya siasa na mikutano ya kisiasa?” amehoji Magereri.

Amesema hivi karibuni Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alizuiliwa kufanya mikutano ya kisiasa lakini Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Humphery Polepole akaruhusiwa kufanya mikutano.

Naye Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Dk Mwigulu Nchemba amesema utaratibu unaotumika kutokuwa na mikutano ya siasa wakati unapomalizika uchaguzi ni standard (viwango) za kimataifa.

“Hakuna nchi wanapomaliza uchaguzi wanaendelea na kampeni. Utaratibu holela umesababisha kupoteza maisha ya Watanzania na familia zilizopoteza ndugu zao hawaziangalii tena,” amesema.

Alisema hakuna sheria iliyovunjwa kuzuia mikutano ya kisiasa nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema anaamini mbunge huyo anazungumzia mikutano ya kampeni hivyo asubiri ratiba inayotolewa na Tamisemi.

“Hawaruhusiwi kufanya bila kibali cha Polisi.  Ni suala la utaratibu tu. Mkuu wa kituo atakutana nao akiona mazingira hayaruhusiwi anawaambia wasifanye mkutano,” amesema.

Ameema kabla ya kutoa kibali wanaangalia vifaa, askari na kuwataka wabunge kufahamu kuwa kuna Sheria ya Jeshi la Polisi.

Kangi amesema haiwezekani kukawa na siku chache za kufanya maendeleo na siku nyingi zikatumika katika mikutano ya kisiasa.

Hata hivyo, akihitimisha hoja yake kabla ya wabunge kupiga kura, Jaffar amesema amani inajengwa na pande zote na kwamba hawajaona sheria inakataza vyama visifanye kazi zake.

Hata hivyo, baada ya wabunge kupiga kura, mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema hoja hiyo imekataliwa.