Benki ya Dunia yatofautiana na Serikali ya Tanzania kukua kwa uchumi

Thursday July 18 2019

Benki Dunia, yatofautiana,  Serikali  Tanzania , kukua uchumi,mwananchi, habari mwananchi

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Tofauti ya makadirio ya Serikali, Benki ya Dunia imesema uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.2 mwaka jana.

Wakati Benki ya Dunia ikisema hayo, taarifa za Serikali ya Tanzania zinaonyesha uchumi uliongezeka kwa asilimia 7.0 mwaka 2018

Akisoma hotuba ya hali ya uchumi wa Taifa mwaka 2018 na mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2019/20 kwenye bungeni la bajeti lililoisha hivi karibuni, waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisisitiza ukuaji wa uchumi wa asilimia 7.0.

Lakini, mchumi mwandamizi wa benki hiyo, Bill Battaile amesema wao wanaamini hali ilikuwa tofauti na msimamo wa Serikali.

“Takwimu za NBS zinaonyesha pato la Taifa (GDP) lilikua kwa asilimia 7.0 lakini Benki ya Dunia inaamini kasi hiyo ilikuwa asilimia 5.2,” amesema Battaile.

Kutokana na tofauti hiyo, mkurugenzi mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alishindwa kuvumilia hivyo akaomba ufafanuzi kwa mtoa hoja.

Advertisement

“Sisi tuliopo ‘field’ tunajua hali halisi. Takwimu zetu zinaonyesha uchumi umekua kwa asilimia 7.0 lakini ninyi mnasema ni asilimia 5.2. Kwa nini tofauti imekuwa kubwa kiasi hicho?” alihoji mtakwimu mkuu wa Serikali.

Akimjibu Dk Chuwa, mchumi wa Benki ya Dunia amesema kiasi hicho cha ukuaji wa uchumi wamekipata kwa kutumia taarifa za wizara ya fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na NBS yenyewe.

Benki ya Dunia si ya kwanza kutoa taarifa inayoonyesha kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi ikilinganishwa na iliyotolewa na Serikali. Mwaka jana, IMF ilisema pato la Taifa linakua kwa asilimia 4.8.

Kutetea hoja hiyo, benki hiyo imesema utegemezi wa Tanzania ulikuwa asilimia mbili ya GDP mwaka 2018/19 huku madeni ya ndani ya Serikali yakiendelea kuongezeka.

Vilevile, Serikali haikukusanya mapato iliyotarajia wala kupeleka fedha ilizoahidi kwenye miradi ya maendeleo huku ulipaji wa marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ukiwa chini.

Kuimarisha uchumi, benki hiyo imeshauri kuboreshwa kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

“Mabadiliko ya ghafla ya sera husababisha kutotabirika  kwa biashara. Serikali iondoe changamoto kwenye nishati, usafiri na miundombinu ya dijiti kuivutia sekta binafsi kuwekeza,” amesema Battaile.

 


Advertisement