ACT kuandamana kushinikiza Bunge lifanye kazi na Profesa Assad

Katibu wa Mawasiliano Ngome ya Vijana, ACT Wazalendo, Karama Kaila  akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.Picha na Said Khamid

Muktasari:

  • Ngome ya Vijana ACT- Wazalendo, Jumanne ya Aprili 9, 2019 watafanya maandamano jijini Dodoma yenye lengo la kulishinikiza Bunge kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa  Assad.

Dar es Salaam. Ngome ya Vijana ACT- Wazalendo wamepanga kufanya maandamano Jumanne ya Aprili 9, 2019 jijini Dodoma yenye lengo la kulishinikiza Bunge kufuta azimio lake la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad.

 Katibu wa Mawasiliano Ngome ya Vijana, ACT Wazalendo, Karama Kaila akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Aprili 7, 2019 katika ofisi za Makao Makuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Kijitonyama jijini Dar es Salaam amesema watafanya maandamano ya amani Aprili 9, 2019.

 Kaila pia amesema kwamba dhumuni la maandamano hayo ni kulishinikiza Bunge kuweka kwenye shughuli zake (Order Paper ) upokeaji wa Taarifa ya CAG ikiwa na saini ya Profesa Assad ifikapo Aprili 10, 2019 saa tatu asubuhi.

 

Amesema wao kama vijana wa ACT-Wazalendo kwa niaba ya mabaraza, jumuiya na ngome za vijana wa vyama vya siasa vya NCCR Mageuzi, CHAUMA, UPDP na vyama vingine vitatu ambavyo vitaungana nao baada ya uamuzi wa vikao vyao vya ndani, watafanya maandamano hayo ya amani mkoani Dodoma siku hiyo.

 

“Tumefikia uamuzi huu baada ya kujiridhisha kwamba uamuzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na Bunge kwa ujumla wake kusitisha kufanya kazi na CAG ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeanzisha Mamlaka ya CAG na kuzuia kabisa kuingiliwa katika majukumu yake na kwamba ni wajibu wa kila raia kuilinda Katiba,” amesema Kaila. 

Amesema kwa Mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Polisi (police ordinance) ambayo inataka kutoa taarifa kwa saa 48 kabla ya muda wa maandamano, umma ufahamu kuwa tayari wamekwisha toa taarifa ya kufanyika kwa maandamano hayo kwa OCD-Dodoma. 

Amebainisha kuwa maandamano hayo yatafanyika Aprili 9, mwaka huu, Jumanne, saa 3:00 asubuhi na kwamba yataanzia Nyerere Square Jijini Dodoma kupitia barabara ya Jamatini na kuingia barabara ya Bunge hadi Jengo la Bunge Jijini Dodoma.

 

Kaila aliongeza kuwa wamemwomba Spika wa Bunge au Naibu Spika apokee maandamano hayo ya  amani.


Pia amewaomba Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama kusimama imara kuilinda misingi ya Katiba yetu kwa kujitokeza kwa wingi kwenda maandamano hayo ya amani yenye kauli Mbiu ya “Tunasimama na CAG. “

  

Hata hivyo, Mwananchi limezungumza na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gilles Muroto na amesema hana taarifa na maandamano hayo.