Alichokisema dereva wa Lissu katika mahojiano Ujerumani
Muktasari:
Adam Bakari, dereva wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema shambulizi walilofanyiwa akiwa pamoja na mbunge huyo lilikuwa likijulikana na kutaka watu kutomhusisha na jambo hilo
Dar es Salaam. Adam Bakari, dereva wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema shambulizi walilofanyiwa akiwa pamoja na mbunge huyo lilikuwa likijulikana na kutaka watu kutomhusisha na jambo hilo.
Amedai ndio maana siku ya tukio hilo Septemba 7, 2017 katika makazi ya mbunge huyo hakukuwa na ulinzi wa aina yoyote.
Bakari ametoa kauli hiyo katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Ujerumani DW Deutsche Welle.
Mbunge huyo alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari, nje ya nyumba yake, Area D mjini Dodoma lakini dereva wake huyo ambaye walikuwa wote hakupatwa na risasi na Lissu mara kadhaa amekuwa akieleza jinsi alivyomsaidia.
Dereva huyo amesema katika eneo ambalo shambulizi lilifanyika hulindwa na askari wenye silaha kila siku ila siku ya tukio hawakuwepo.
“Lakini mbona mimi sikujificha baada ya tukio na tuliwaambia kama wanataka kunihoji waje Nairobi mbona hawakufanya hivyo licha ya muda wote niliokuwepo pale,” amesema Bakari.
Akisimulia tukio hilo amesema siku hiyo walikuwa wakitokea bungeni kurudi katika eneo wanaloishi ndipo aligundua kwa nyuma kuna magari mawili yanawafuatilia.
“Nilipoona yapo nyuma yetu kwa muda nikaona bora niyapishe lakini hayakupita hivyo nikakunja kona ya kwanza nikaona gari bado zipo, nikakunja kona ya pili zipo nikaona hizi gari sio salama kwetu na nikaamua kuongeza mwendo,” amesema Bakari.
“Wakati huo sikumwambia chochote bosi (Lissu). Tukafika karibu na nyumbani kuna ‘club’ inaitwa ‘84’ gari iliyokuwa inanifuatia mimi ni V8 (Toyota) ikapaki pembeni ile Nissan iliyokuwa nyuma yake ilikuja kwa speed (kasi) kunifuata mimi nilipoingia getini na yenyewe iliingia.”
Ameongeza, “Tukapaki gari na wenyewe wakapaki wakiwa wamevaa kofia na miwani wakawa wanazungumza pale bila sisi kusikia. Walipomaliza gari ilirudi nyuma speed na ilipofika usawa wa gari yetu ilisikika tu milio ya risasi.”
Amesema aliposikia kelele za milio ya risasi na kelele za Lissu aliyekuwa ameketi upande wa kushoto, alifungua mlango wa gari upande wa kulia na kumvuta mbunge huyo nje.
Amesema wakati akifanya jambo hilo risasi zilikuwa zikiendelea kumiminwa katika gari hilo, “mimi nilichanwa na vioo katika baadhi ya maeneo.”