Asimulia jinsi alivyomaliza waganga kutibu saratani

Pamoja na Serikali kuendelea kuhamasisha kuwahi hospitali unapoona mabadiliko ya kiafya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu, lakini bado wapo watu wanaohangaika kutibu magonjwa makubwa kwa dawa za kienyeji.

Hali hiyo imekuwa ikichangia wengi kupoteza maisha au kwenda hospitalini ugonjwa ukiwa katika hatua mbaya ambayo haiwezi kutibika au matibabu yake kuhitaji fedha nyingi.

Waishio vijijini ndio waathirika wakubwa katika hili kama ilivyomtokea Hamis Juma.

Huyu ni mtoto wa miaka minne ambaye kwa miezi sita sasa maisha yake yamekuwa ndani ya Kituo cha Tumaini la Maisha kilichopo kwenye viunga vya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) anakopatiwa matibabu ya saratani ya tezi shingoni.

Ugonjwa huo ulimuanza Hamis kama uvimbe, ukaendelea kukua na hatimaye kutengeneza kidonda kilichodumu kwa muda mrefu bila kupona.

Baba wa mtoto huyo, Juma Nzoya ambaye ni mwenyeji wa Kijiji cha Kasimbe wilayani Momba mkoani Songwe aligundua kwamba mwanae kuwa na tatizo hilo miaka miwili iliyopita, lakini alikuwa akimtibu kwa njia za kienyeji.

Akizungumza na Mwananchi kituoni hapo, Nzoya anaeleza kuwa baada ya kugundua tatizo hilo alijaribu kumtibia kwa kumpaka majani na dawa za mitishamba lakini hakupata nafuu.

Hali hiyo ikamsukuma kuanza kuomba ushauri kwa watu ndipo alipokutana na waganga wa kienyeji ambao kila mmoja alijaribu utaalamu wake kumsaidia mtoto huyo bila mafanikio.

“Kuna mmoja aliniambia tuwe tunatumia kitunguu saumu akidai kuwa kinasaidia. Nikawa nampaka kila siku lakini bado hatukuona mabadiliko na badala yake uvimbe ukazidi kuwa mkubwa.

“Mganga mwingine aliniambia nimpe Sh50,000 ili auhamishe ule uvimbe kutoka shingoni hadi tumboni kisha ataharisha, nilifanya hivyo akampa na hizo dawa lakini hakuna lililobadilika bali mtoto akazidi kudhoofika,” anasema.

Nzoya anasema aliendelea na hali hiyo akiamini kuwa ipo siku mtoto wake angepona na kurejewa na afya yake kama kawaida kwa dawa za kienyeji.

Machi mwaka huu akaona hakuna mabadiliko kwa mtoto wake na hali inazidi kuwa mbaya baada ya kumuona anazidi kukonda na kupoteza nuru ndipo akapata wazo la kumpeleka hospitali ya Vwawa mkoani Songwe.

Huko alipatiwa huduma ambazo hata hivyo hazikumsaidia hali iliyomlazimu kumpeleka Hospitali ya Rufaa Mbeya ambako alifanyiwa vipimo.

Baada ya uchunguzi kufanyika kwa kina ilibainika kuwa tatizo la Hamis linakaribiana na saratani hivyo akahamaishiwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Huko ilithibitika kwamba ana saratani ya tezi ya shingo ugonjwa ambao ulimuanza muda mrefu.

Anasema mara moja mtoto huyo akaanzishiwa matibabu lakini alipoanza kupata nafuu akaruhusiwa kurejea nyumbani huku akiendelea na dawa za mionzi anazotakiwa kupata kila wiki.

Kutokana na kukosa makazi jijini Dar es Salaam, Hamis anaendelea kupatiwa matibabu MNH na kuishi kwenye kituo hicho ambacho ni makazi maalumu kwa ajili ya watoto wanaougua saratani wanaotokea mikoani.

Kiongozi wa kituo hicho, Hilda Mwageni anaeleza kuwa mara kwa mara wamekuwa wakipokea wagonjwa waliopitia safari kama ya Hamis hali inayoashiria bado kuna watu hawana uelewa wa kutosha na wanaamini dawa za kienyeji.

Anasema kituo hicho chenye jumla ya vyumba 11 kina uwezo wa kuchukua watoto 22 kwa maana ya kila chumba kimoja kuwa na vitanda viwili ambapo kila mtoto hulala na mzazi wake.

Pamoja na mambo mengine mengi Mwageni anaeleza kuwa kituo hicho kina uhaba wa mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa ajili ya watoto na wazazi hao, hivyo akatoa wito kwa wanaoguswa wawasaidie.

Wakiitikia wito huo, hivi karibuni wafanyakazi wa kampuni ya upimaji na upangaji ardhi ya Husea walifanya ziara kwenye kituo hicho na kuchangia baadhi ya mahitaji muhimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Pamela Maro anasema kuguswa kwao kukisaidia kituo hicho kumetokana na kazi kubwa inayofanywa katika kunusuru maisha ya watoto wenye saratani.

“Tunafahamu kazi kubwa inayofanyika hapa, niwapongeze wahudumu na wazazi wote kwa kuwa pamoja na watoto hawa ambao wamepata mitihani wakiwa katika umri mdogo,

“Kuonyesha tupo pamoja nanyi tumeona tuwaletee vitu vichache ambavyo vitakusaidieni katika kipindi hiki. Niwasihi wazazi msikate tamaa ili mradi mmefika hospitali mmenusuru maisha ya watoto wenu,” anasema Maro.