Bajeti ya Zanzibar 2019/20 ni Sh1.41 trilioni

Thursday June 20 2019

 

By Haji Mtumwa,Mwananchi [email protected]

Unguja. Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa amesema mwaka wa fedha 2019/20 Serikali ya Zanzibar imekadiria kutumia Sh1.419 trilion.

Amesema makadirio hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.9 ya makadirio ya Sh1.315 trilion ya mwaka 2018/19.

Balozi Ramia amesema hayo leo Alhamisi Juni 20, 2019 katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi wakati akiwasilisha hotuba ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2019/20.

Amesema kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida ni Sh842.4 bilioni, matumizi ya maendeleo Sh577.0 bilioni, ambapo utegemezi wa bajeti unatarajiwa kuongezeka na kufikia asilimia 6.2 kutoka asilimia 5.7 ya mwaka 2018/19.

Balozi Ramia amesema hali hiyo imechangiwa na kuimarika kwa mapato ya ndani na kuongezeka kwa ruzuku kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Amesema kwa mwaka 2019/20 Serikali inatarajia kukusanya Sh1.419 bilioni zikiwemo Sh 976.5 bilioni zitokanazo na vyanzo vya ndani na Sh394.6 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo, Sh40 bilioni mikopo ya ndani, Sh8.3 bilioni mifuko ya wafadhili.

Advertisement

Balozi Ramia amesema kati ya Sh976.5 bilioni zitokanazo na makusanyo ya mapato ya ndani Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) inatarajiwa kukusanya Sh488.5 bilioni, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tawi la Zanzibar inatarajiwa kukusanya Sh350.2 bilioni, mapato ya wizarani Sh116.8 bilioni na kodi ya mapato ya wafanyakazi wa SMT Sh 21 bilioni.

Amesema kuhusu mapato ya nje ya Sh394.6 bilioni kutoka kwa washirika wa madeleo waziri huyo amesema mapato hayo yanajumuisha kutokana na ruzuku ya Sh95.5 bilioni na mikopo ya Sh296.1 bilioni.

 

 


Advertisement